Q Chief: Hata Diamond, Ali Kiba na Marioo hawaniwezi kunishinda Live

DAR ES SALAAM: MSANII mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva, Abubakary Katwira ‘Q Chief’, ameibua mjadala baada ya kujigamba kuwa hakuna msanii nchini anayeweza kumzidi uwezo wa kuimba moja kwa moja (live).
Q Chief amesema uwezo wake wa kuimba live ni kipaji alichobarikiwa na Mungu, akisisitiza kuwa hata wasanii wakubwa kama Diamond Platnumz, Ali Kiba, Marioo na Jay Melody wakikusanyika pamoja, bado hawawezi kumshinda katika uimbaji wa moja kwa moja.
Akizungumzia uwezo wake wa muziki, Q Chief amesema kutajwa msanii mmoja mmoja kuwa anaweza kumshinda ni kumshusha thamani, kwani anaamini uwezo wake wa kuimba live uko katika kiwango cha juu.
“Sasa hivi nilipofikia, ndugu Watanzania, mpango wa kunitajia msanii mmoja mmoja kwamba nitamfunika ni kunishusha daraja na thamani yangu. Chukua Diamond, chukua Ali Kiba, chukua Marioo, chukua Jay Melody, chukua familia yako nzima.
Mkiweza kunifunika, nitaamini kweli Tanzania kuna wasanii,” amesema Q Chief.
Amesema kipaji chake cha kuimba moja kwa moja ni sehemu ya uwezo alioupata kutoka kwa Mungu, akieleza kuwa anajivunia kiwango alichofikia katika muziki.
Kauli hiyo imeibua mjadala miongoni mwa mashabiki wa Bongo Fleva, huku baadhi wakijadili uwezo wa wasanii mbalimbali katika uimbaji wa moja kwa moja na wengine wakitazama kauli ya Q Chief kama changamoto kwa wasanii wenzake.
Q Chief ni miongoni mwa wasanii waliotoa mchango mkubwa katika muziki wa Bongo Fleva, huku uwezo wake wa kuimba na kufanya maonesho ya moja kwa moja ukiendelea kuwa sehemu ya mjadala miongoni mwa mashabiki wa muziki huo.




