Ligi Kuu

Simba, Singida wanatoleana macho

SINGIDA:SIMBA na Singida zinatarajia kucheza kesho katika mchezo wa Ligi Kuu mzunguko wa tatu kwenye Uwanja wa Airtel mkoani Singida.

Mchezaji wa Simba Antony Mligo, amesema wamejiandaa vizuri kukabiliana na wapinzani hao na lengo lao ni kuondoka na pointi tatu.

Mligo amesema wanatambua ubora wa Singida, lakini Simba imejiandaa kupambana kuhakikisha inapata ushindi katika mchezo huo.

“Tunajua umuhimu wa mchezo dhidi ya Singida. Ni timu nzuri, lakini sisi kama wachezaji tumejiandaa vizuri na tunajua namna ya kuingia uwanjani na kupambana ili kupata alama tatu muhimu,” amesema Mligo.

Kwa upande wa Singida Black Stars Kocha Mkuu Kimoto Papy amesema mchezo dhidi ya Simba SC ni mkubwa kwa pande zote mbili, huku akisisitiza kuwa kikosi chake kimejikita katika kurejesha nguvu za wachezaji na kujiandaa kiakili ili kupigania pointi tatu.

Kocha huyo amesema timu zote zimetoka kucheza michezo yao siku mbili zilizopita, hivyo muda wa maandalizi umekuwa mfupi, huku safari ikiwa imeongeza changamoto katika maandalizi.

“Ni mchezo mkubwa sana kwa pande zote mbili. Ukitazama, tumetoka kucheza siku mbili zilizopita, sisi Singida pamoja na Simba. Kwa sasa jambo la msingi ni kuhakikisha hali za wachezaji ziko vizuri kuelekea mchezo huu wa nyumbani kwa sababu ni mchezo mkubwa na tunahitaji kufanya vizuri ili kupata alama tatu,” amesema.

Ameongeza kuwa Simba ni miongoni mwa timu kubwa nchini, hivyo maandalizi ya mchezo huo yanahitaji wachezaji kuwa tayari kimwili na kiakili.

Related Articles

Back to top button