Kocha wa Yanga atamba watafunga sana

DAR ES SALAAM:KOCHA Mkuu wa Yanga Manqoba Mngqithi amesema bado anaona nafasi ya kikosi chake kufunga mabao mengi zaidi licha ya kufikisha mabao saba katika michezo miwili, akisisitiza kuwa timu yake bado iko kwenye hatua ya kujijenga na wachezaji wanaendelea kuzoea mfumo wake.
Akizungumza baada ya mchezo dhidi ya Coastal Union amesema timu yake ilitawala sehemu kubwa ya mchezo na ilitengeneza nafasi nyingi, lakini amekiri kutoridhishwa na namna walivyoruhusu bao katika ushindi wao wa mabao 4-1.
“Sitaki kuruhusu mabao. Nafikiri ni mchezo ambao tungeweza kufunga hata mabao sita kipindi cha kwanza na matano kipindi cha pili. Lakini timu bado inakua na wachezaji bado wana presha kwa sababu kila mmoja anataka kunithibitishia kitu,” amesema.

Kocha huyo amesema kwake jambo kubwa ni kushinda michezo na kufunga mabao, akieleza kuwa mabao saba katika michezo miwili ni matokeo mazuri, lakini kikosi chake bado kina uwezo wa kufanya vizuri zaidi.
“Natamani kushinda michezo na kufunga mabao. Mabao saba katika michezo miwili ni matokeo mazuri, lakini bado tunaweza kufanya vizuri zaidi kwa sababu katika michezo yote miwili hatukutumia nafasi zetu vizuri,” amesema.
Akizungumzia mabadiliko aliyofanya baada ya timu yake kuongoza mabao 3-0, kocha huyo amesema alimuingiza mchezaji kwa kuamini uwezo wake wa kupiga krosi na kusaidia washambuliaji kupata nafasi za kufunga.
Amesema anataka washambuliaji wake waanze kufunga mapema ili kujenga kujiamini na kuondokana na presha inayowakabili mwanzoni mwa msimu.
Kuhusu kiwango cha Chadrack Boca, kocha huyo amesema ameridhishwa na kiwango chake, akimsifu kwa juhudi na kufanya kazi kwa bidii tangu kipindi cha maandalizi ya msimu.




