Ibenge: Tulijua TRA itakuwa ngumu

DAR ES SALAAM: KOCHA M wa Azam FC, Florent Ibenge, amesema alifahamu mapema kuwa mchezo dhidi ya TRA United ungekuwa mgumu kutokana na namna wapinzani wao wanavyocheza, lakini amefurahishwa na ushindi wa mabao 2-1 walioupata jana kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Ibenge amesema Azam ilicheza vizuri kipindi cha kwanza, kabla ya kupoteza umakini mwanzoni mwa kipindi cha pili na kuruhusu TRA kupunguza bao, hali iliyoufanya mchezo kuwa mgumu zaidi hadi mwisho.
“Wao wanashambulia kama sisi na wanajilinda kama sisi, hivyo nilijua ungekuwa mchezo mgumu. Tulicheza kipindi cha kwanza vizuri sana, lakini mwanzoni mwa kipindi cha pili tulipoteza umakini. Unapoongoza 2-0 halafu mpinzani akafunga na kufanya 2-1, mchezo unakuwa mgumu.
“Tulipambana, lakini kwa bahati mbaya tukapata kadi nyekundu, hivyo mambo yakawa magumu zaidi. Hata hivyo, ni vizuri kwamba tuliweza kulinda matokeo na kupata pointi tatu za kwanza za msimu. Tunafurahi,” amesema Ibenge.
Kwa upande wake, kocha wa TRA United, Ettiene Ndayiragije, amesema licha ya timu yake kupoteza mchezo huo, haikuwa rahisi kwa Azam kupata ushindi kutokana na namna walivyocheza na kutengeneza nafasi.
“Sio kwamba wao walipata nafasi nyingi. Sisi bado tulitengeneza nafasi, tulimiliki sana mipira. Ukiangalia video, ukiangalia tulifika mara kadhaa kwenye eneo lao na tulipata nafasi za kufunga,” amesema Ndayiragije.
Ndayiragije amesisitiza kuwa matokeo hayabadilishi mtazamo wake kuhusu uwezo wa kikosi chake, akiamini timu hiyo itajifunza kutokana na makosa yaliyojitokeza katika mchezo huo na kurejea kwa nguvu katika michezo inayofuata.




