Mgunda akiri bado hawajakaa sawa

LINDI: KOCHA Mkuu wa Namungo Juma Mgunda amesema ushindi wa bao 1-0 uliopatikana kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Geita ulikuwa muhimu kutokana na ushindani mkubwa wa ligi, lakini amesisitiza kuwa timu yake bado ina mambo ya kuyafanyia kazi kabla ya mchezo unaofuata.
Mgunda amesema timu yake ilitawala mchezo kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha kwanza, lakini wapinzani wao walibadilika kipindi cha pili na kumiliki mpira zaidi, hali aliyosema ilichangiwa na presha ya kutafuta matokeo.
“Alhamdulillah, mechi imekwisha, tumeshinda. Utaona tulimiliki mpira kwa kiasi kikubwa sana kipindi cha kwanza, lakini kipindi cha pili wenzetu pia walimili mpira kwa kiasi kikubwa. Yote ni kwa sababu ya presha ya kutaka matokeo,” amesema.
Amesema licha ya kupata ushindi, kikosi chake kina mambo mazuri pamoja na mapungufu ambayo wanapaswa kuyafanyia kazi, hasa kutokana na ratiba kuwa ngumu ambapo baada ya siku mbili wanatarajiwa kucheza mchezo mwingine.
Kocha huyo amesema baada ya kupata ushindi huo, jambo la msingi ni kuendelea kuwa karibu na wachezaji, kuzungumza nao kuhusu mapungufu yaliyobainika na kujiandaa kwa changamoto zinazowakabili katika michezo ijayo.




