Ligi Kuu

Fountain Gate, Mashujaa kusaka pointi tatu leo

ARUSHA: FOUNTAIN Gate FC itakuwa na kibarua cha kuwarekebishia Mashujaa FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara mzunguko wa pili kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.

Mchezo huo utachezwa saa 10:00 jioni. Fountain Gate inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na jukumu la kusahihisha makosa yaliyojitokeza katika mechi yake ya kwanza ya msimu, baada ya kupoteza mabao 3-0 dhidi ya Singida Black Stars.

Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Fred Minziro, amesema maandalizi ya timu yake yamekwenda vizuri na wachezaji wake wako tayari kupambana kupata matokeo mbele ya mashabiki wao.

Kwa upande wake, mchezaji wa Fountain Gate, Sadick Ramadhan, amesema wanaelewa umuhimu wa mchezo huo, hasa baada ya kushindwa kupata matokeo mazuri katika mchezo wao wa kwanza wa ligi.

“Kama wachezaji tunatambua tunahitaji kubadilisha hali hiyo kwa kupata matokeo chanya dhidi ya Mashujaa,”amesema.

Mashujaa, chini ya kocha Aman Josia, wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na morali baada ya kuanza msimu kwa ushindi wa ugenini wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union.

Aman amekiri mchezo huo utakuwa na ugumu kutokana na kucheza na Fountain Gate ikiwa nyumbani na ikiwa inatafuta matokeo baada ya kupoteza mchezo wake wa kwanza, lakini amesema wachezaji wake wameandaliwa kukabiliana na changamoto hiyo bila kuacha ubora waliouonesha katika maandalizi ya msimu na mchezo wao wa kwanza.

Katika mchezo mwingine wa ligi, Namungo FC itakuwa mwenyeji wa Geita Gold FC kwenye Uwanja wa Majaliwa saa 1:00 usiku, huku timu hizo zikiingia zikiwa na matokeo tofauti katika mechi zao za kwanza.

Namungo ilianza msimu kwa kupoteza mabao 3-1 dhidi ya Yanga huku Geita Gold ikitoka kushinda ugenini bao 1-0 dhidi ya Mbeya City.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button