Davido amalizana na Sony Music

LAGOS: MKALI wa Afrobeats, Davido ametangaza kuachana na Lebo ya Sony Music na albamu mpya ya Oriade ndio ushirikiano wao wa mwisho.
Davido amelieleza hilo punde baada ya juzi kuachia albamu yake hiyo ya sita yenye nyimbo 13.
Video iliyomuonyesha akiwa na ‘streamer’ maarufu wa Nigeria, Carterefe ilithibitisha hilo, aliposema: “Hii ndio albamu yangu ya mwisho kufanya kazi na Sony… Sasa naangalia uelekeo mwingine, ikiwa ni awamu nyingine katika kazi yangu. Niko huru!”
Tamko hilo la Davido linahitimisha ushirikiano wake wa miaka 10 na kampuni hiyo kubwa ya muziki duniani, ulioanza mwaka 2016 kupitia RCA Records.
Aidha, siku chache nyuma kabla ya kuachiwa Oriade, msanii huyo aliangusha ‘party’ ya nguvu mjini New York kwa ajili ya kusikiliza ngoma zake 13 za albamu hiyo.
Usiku huo alikuwa na mkewe, Chioma, DJ Ecool na meneja wake, Asa Asika kabla ya baadae kujumuika kutumbuiza na mastaa wengine waliojitokeza akiwemo Black Sherif aliyemshirikisha kwenye ngoma ya Amazing Grace unaopatikana kwenye Oriade pia.
Mbali na Sherif kutoka Afrika Kusini, wengine walioshirikishwa kwenye albamu hiyo ni Leon Thomas, Aya Nakamura, Mayorkun, Fola, Llona, NO11, JAZZWRLD, na GL Ceejay.




