Praise: Utukufu wote ni wa Mungu, sitapunguza kasi baada ya ushindi wa BSS

DAR ES SALAAM: MSHINDI wa shindano la Bongo Star Search 2026, Praise Wisdom, amesema ushindi alioupata ni matokeo ya neema ya Mungu na sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wake, huku akiahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii katika safari yake ya muziki.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Praise amesema bado haamini ndoto yake ya kushinda shindano hilo imetimia, akieleza kuwa Mungu alimpa nguvu katika kila hatua ya mashindano, kuanzia usaili, mazoezi hadi nyakati alizokuwa akijitilia shaka.
“Utukufu wote ni wa Mungu. Bado siamini. Kushinda CRDB Bongo Star Search 2026 ni ndoto ambayo kwa muda mrefu nilikuwa naiota, na leo imekuwa kweli. Mungu ameniongoza katika kila hatua. Kwake pekee na iwe sifa na utukufu wote,” ameandika.
Aidha, amewashukuru mashabiki wake kwa kumpigia kura, kumpigia simu na kuendelea kumuunga mkono katika kipindi chote cha mashindano.
“Ushindi huu si wangu peke yangu, ni wetu sote. Upendo wenu ulinipa nguvu ya kuendelea pale nilipohisi kuchoka,” amesema.
Praise pia ametoa shukrani kwa mwanzilishi na timu nzima ya Bongo Star Search kwa kuandaa jukwaa linalowapa vijana wenye vipaji nafasi ya kutimiza ndoto zao.
Vilevile, amemshukuru Jaji Mkuu wa shindano hilo, Madam Rita Paulsen, pamoja na majaji Salama Jabir, Master Jay, Meena Ally, Coy Mzungu na S2Kizzy kwa ushauri na mafunzo waliyompa katika kipindi chote cha mashindano.
Akizungumzia hatua inayofuata baada ya ushindi huo, Praise amesema anaupokea kwa unyenyekevu na kuahidi kuwa huo ni mwanzo wa safari yake ya mafanikio.
“Ninapokea ushindi huu kwa unyenyekevu mkubwa. Huu ni mwanzo tu. Nina mengi zaidi ya kuwapa, na safari ndiyo inaanza. Sitapunguza kasi,” amesema.




