Azam yapigwa faini ya Sh. milioni 50

DAR ES SALAAM: KAMATI ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeitoza Azam FC faini ya Sh milioni 50 baada ya klabu hiyo kukataa kushiriki kwenye sherehe za kukabidhiwa tuzo na zawadi kufuatia fainali ya Kombe la Shirikisho la Benki ya CRDB iliyochezwa Julai 4, 2026, Uwanja wa Gombani, Pemba.
Katika mchezo huo wa fainali uliochezwa hivi karibuni Zanzibar, Simba ilishinda bao bao 1-0.
Mbali na adhabu hiyo, Kamati hiyo pia imemfungia kocha wa makipa wa Azam FC, Roudy Mountaro, michezo minne na kumtoza faini ya Sh milioni mbili kwa kosa la kumshambulia mwamuzi baada ya filimbi ya mwisho.
Aidha, golikipa wa Azam FC, Zuberi Foba, amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Sh milioni mbili kwa kosa hilo hilo la kumshambulia mwamuzi baada ya mchezo kumalizika.
Kwa mujibu wa taarifa ya TFF iliyotolewa na Ofisa Habari na Mawasiliano, Cliford Ndimbo, adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni mbalimbali za TFF zinazohusu nidhamu kwa klabu, makocha na wachezaji.
Wakati huohuo, Kamati ya Mashindano imewapeleka kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kiongozi wa Azam FC, Jamal Mohamed (Bui), pamoja na Ofisa wa Simba SC, Ally Shatry (Chico), ili wafanyiwe uchunguzi na kuchukuliwa hatua kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyodaiwa kufanywa katika mchezo huo wa fainali.
Mwisho




