AFCONAfrica

Gomes awaza makundi Afrika

KOCHA Mkuu wa Simba, Didier Gomes amesema mazoezi wanayoendelea nayo yanampa matumaini ya kufanya vizuri na kutinga hatua ya makundi kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwenang Galaxy ya Botswana.

Simba inajifua katika Uwanja wa MO Arena, Bunju Dar es Salaam, na juzi ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya kituo cha Cambiaso na kuibuka na ushindi wa mabao 4-1.

Akizungumza na gazeti hili, Gomes alisema uwajibikaji wa wachezaji wake mazoezini ndiyo siri ya kuelekea mchezo huo wa kimataifa utakaochezwa ugenini Oktoba 15 na lengo lake ni kushinda idadi kubwa ya mabao ili kujiwekea urahisi kwenye mchezo wa marudiano.

“Mazoezi yanaendelea vizuri na wachezaji wanatimiza majukumu yao ipasavyo na hata wale waliopo kwenye timu za taifa nao nafuatilia maendeleo yao, ukweli naridhika sababu wengi wanapata nafasi za kucheza na wameonesha uwezo,” alisema Gomes.

Kocha huyo, raia wa Ufaransa alisema mechi waliyocheza juzi dhidi ya vijana wa Cambiaso imemsaidia kujua namna wachezaji wake walivyoshika maelekezo ambayo amekuwa akiwapa kwenye mazoezi ya kila siku.

Gomes alisema kabla ya kwenda Botswana wanatarajia kucheza mechi nyingine ya kirafiki ambayo itampa taswira kamili kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao ameupa uzito mkubwa.

Simba ndio timu pekee kwa sasa inayopeperusha bendera ya Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya watani zao Yanga kutolewa mapema hatua ya awali na timu ya Rivers United ya Nigeria mwezi uliopita.

Related Articles

Back to top button