Marekani yatolewa kwa aibu, Ubelgiji yatinga robo fainali

SEATTLE: Ndoto ya Marekani ya kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza imefikia tamati baada ya kuchapwa mabao 4-1 na Belgium katika hatua ya 16 Bora, matokeo yaliyoipeleka Ubelgiji robo fainali kukutana na Hispania.
Marekani, ambao walikuwa wakicheza mbele ya mashabiki wao, walionekana kupoteza mwelekeo tangu dakika za mwanzo, huku Ubelgiji ikitumia makosa ya safu ya ulinzi kuandika ushindi mnono. Huu ni miongoni mwa vipigo vikubwa zaidi kwa Marekani katika Kombe la Dunia tangu mwaka 1990.
Charles De Ketelaere aliifungia Belgium mabao mawili, huku Hans Vanaken na Romelu Lukaku wakiongeza mengine mawili. Bao pekee la Marekani halikuweza kubadili mwelekeo wa mchezo, kwani waliruhusu kufungwa tena muda mfupi baada ya kusawazisha.
Kabla ya mchezo, mjadala mkubwa ulitawala kuhusu mshambuliaji Folarin Balogun, ambaye aliruhusiwa kucheza licha ya kupewa kadi nyekundu katika mechi iliyopita baada ya adhabu yake kusimamishwa na FIFA. Uamuzi huo ulizua ukosoaji mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali wa soka duniani.
Hata hivyo, kocha wa Marekani, Mauricio Pochettino, alikataa kutumia sakata hilo kama kisingizio cha kushindwa.
“Haikuathiri kiwango chetu. Hii haikuwa siku yetu. Tulianza vibaya na hatukuwahi kuingia vizuri kwenye mchezo,” amesema Pochettino.
Kocha huyo aliongeza kuwa timu yake ilishindwa kuonesha makali yaliyowawezesha kufika hatua ya mtoano, huku makosa ya ulinzi yakiiwezesha Ubelgiji kutawala mchezo.
Kwa upande wake, kocha wa Ubelgiji, Rudi Garcia, amesema Balogun hakupaswa kulaumiwa kwa sakata la kadi nyekundu, akifichua kuwa alimfariji mshambuliaji huyo baada ya mchezo.
Kutolewa kwa Marekani kunawaacha wenyeji wote watatu wa mashindano hayo – Marekani, Canada na Mexico – wakiwa wameishia hatua ya 16 Bora.
Nahodha wa Marekani, Tyler Adams, amesema licha ya maumivu ya kuondolewa, anaamini safari yao imechangia kuongeza hamasa ya mchezo wa soka nchini humo.
“Hatukufika tulipotamani, lakini kama tumewahamasisha watoto wachache kuupenda mchezo huu, basi tumefanikisha jambo muhimu,” amesema Adams.
Sasa macho yataelekezwa kwa mustakabali wa Pochettino, ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mashindano hayo. Kocha huyo amesema atafanya mazungumzo na Shirikisho la Soka la Marekani katika wiki zijazo kabla ya kuamua hatua yake inayofuata.




