Rais Samia amjulia hali Pacome Aga Khan, ampa pole

DAR ES SALAAM: Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amemtembelea na kumpa pole kiungo wa Yanga, Pacome Zouzoua, ambaye anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, kufuatia majeraha aliyoyapata katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya JKT Tanzania.
Rais Samia alipata fursa ya kumjulia hali Pacome alipokuwa hospitalini hapo kumtembelea Sheikh Rashid Hamad Othman, mlezi wa Mwenyekiti wa Taifa wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ambaye pia anaendelea kupatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, baada ya kufahamishwa kuwa mchezaji huyo wa Yanga alikuwa amelazwa katika chumba jirani, Rais Samia aliamua kwenda kumtembelea na kumfariji, akimtakia nafuu ya haraka ili arejee uwanjani kuendelea na majukumu yake.
Pacome alipata majeraha hayo katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu kati ya Yanga na JKT Tanzania uliochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, na tangu hapo amekuwa akiendelea na matibabu chini ya uangalizi wa madaktari.




