Pulisic: Tulionyesha Uimara Hata Baada ya Kubaki Wachezaji 10

CALIFORNIA: Nahodha wa Marekani, Christian Pulisic amesema ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Bosnia-Herzegovina umeonesha uimara wa kikosi chao baada ya kumaliza sehemu kubwa ya mchezo wakiwa pungufu kufuatia kadi nyekundu aliyopewa mshambuliaji Folarin Balogun.
“Tulilazimika kupambana kwa nguvu ili kupata ushindi huu. Mambo hayakwenda kama tulivyopanga baada ya kadi nyekundu, lakini hiyo inaonyesha jinsi tulivyo timu imara. Tulikubaliana wakati wa mapumziko mafupi kwamba huu ndio wakati wa kuonyesha tabia ya mabingwa, na tulifanikiwa kufanya hivyo,” alisema Pulisic.
Marekani imefuzu hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia baada ya kuishinda Bosnia-Herzegovina katika mchezo uliochezwa jijini California.
Balogun aliifungia Marekani bao la kwanza dakika ya 45, likiwa ni bao lake la tatu kwenye mashindano hayo, kabla ya kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 62 baada ya mwamuzi Raphael Claus wa Brazil kupitia tukio hilo kwa msaada wa VAR na kubaini alimkanyaga beki wa Bosnia, Tarik Muharemovic.
Kutokana na adhabu hiyo, Balogun ataukosa mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Belgium, jambo ambalo ni pigo kwa Marekani kwani ndiye kinara wao wa mabao kwenye Kombe la Dunia.
Licha ya kucheza na wachezaji 10, Marekani iliendelea kutawala mchezo na Malik Tillman alihitimisha ushindi huo kwa kufunga bao la pili kwa mpira wa adhabu dakika ya 82, likiwa bao lake la kwanza kwenye Kombe la Dunia.
Beki Chris Richards alisema kikosi hicho kina uwezo wa kuziba pengo la mchezaji yeyote atakayekosekana.
“Mchezaji mmoja akitoka, mwingine anasimama. Hivyo ndivyo ilivyokuwa hata tulipopoteza wachezaji wengine hapo awali. Sisi ni timu, si kutegemea mchezaji mmoja,” alisema Richards.
Kwa ushindi huo, Marekani imeandika historia kwa kushinda mchezo wake wa pili pekee wa hatua ya mtoano kwenye Kombe la Dunia na wa kwanza tangu mwaka 2002. Sasa itakutana na Belgium katika hatua ya 16 bora, ikiwa na matumaini ya kulipa kisasi baada ya kutolewa na wapinzani hao kwenye Kombe la Dunia la mwaka 2014.




