Kwingineko

John Terry: Kukosekana kwa Nigeria kombe la Dunia ni pengo kubwa

NGULI wa zamani wa England na Chelsea, John Terry, amesema kutokuwepo kwa Nigeria kwenye Kombe la Dunia 2026 ni pigo kubwa kwa mashindano hayo, akisisitiza kuwa taifa hilo lina historia kubwa ya soka na lingeongeza ushindani mkubwa.

Nigeria ilikosa nafasi ya kufuzu baada ya kumaliza nyuma ya Afrika Kusini katika hatua ya makundi ya kufuzu kwa ukanda wa Afrika kabla ya kushindwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa mikwaju ya penalti katika mchezo wa mtoano ulioamua nafasi ya mwisho.

Matokeo hayo yameifanya Nigeria kukosa Kombe la Dunia kwa mara ya pili mfululizo baada ya pia kukosekana kwenye mashindano ya mwaka 2022 yaliyofanyika nchini Qatar.

Akizungumza katika kikao cha mtandaoni kilichoandaliwa na SuperSport, Terry alisema ni jambo la kusikitisha kuona taifa lenye vipaji vikubwa kama Nigeria likikosekana kwenye mashindano hayo.

Alisema Nigeria imekuwa moja ya mataifa yenye uwezo mkubwa wa kufika mbali kutokana na ubora wa wachezaji wake na uzoefu wake kwenye mashindano makubwa.

Kwa mujibu wa Terry, Kombe la Dunia huwa jukwaa la kuonesha ubora wa timu bora duniani, hivyo kutokuwepo kwa Nigeria kunaacha nafasi ambayo mashabiki wengi wangependa kuiona ikipewa ushindani mkubwa zaidi.

Terry pia alitania kuwa mmoja wa waliovunjika moyo ni kiungo wa zamani wa Nigeria John Obi Mikel ambaye angependa kuona taifa lake likiwepo kwenye mashindano hayo.

Kombe la Dunia 2026 linaanza rasmi leo kwa mchezo wa ufunguzi kati ya Mexico na Afrika Kusini, huku macho ya dunia yakielekezwa kwenye historia mpya ya mashindano hayo makubwa zaidi kuwahi kufanyika.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button