Højlund mchezaji bora EPL Februari

MSHAMBULIAJI Rasmus Højlund amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu England(EPL) mwezi Februari kufuatia nyota huyo wa Manchester United kufunga mabao mfululizo.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Denmark amekuwa na kiwango bora katika wiki za hivi karibuni akifunga katika michezo yote sita iliyopita aliyocheza kabla ya kuumia msuli.
Alisajiliwa toka Atalanta ya Italia kwa pauni mil 72.
“Nina furaha sana. Kwa kweli, ni bahati kubwa kupata tuzo hii, hasa kutokana na kuwepo washindani wengine kwenye kinyang’anyiro pia,’ amesema Højlund kwenye tovuti ya klabu hiyo.
Wakati huo huo Kocha wa Arsenal Mikel Arteta amechaguliwa kuwa kocha bora kutokana na klabu hiyo kuwa na mwenendo usiotetereka mwezi Februari.
Arteta ni kocha pekee ambaye timu yake haijapoteza mchezo Februari, matokeo yaliyosaidia klabu hiyo kupunguza pengo kati yake na Liverpool na Manchester City katika msimamo wa EPL hadi pointi mbili.