Haji Manara: Hatuendi Morocco kufanya siasa

DAR ES SALAAM:MSEMAJI wa timu za taifa za soka nchini, Haji Manara, amesema safari ya Watanzania zaidi ya 100 kuelekea Morocco kwa ajili ya fainali ya Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U-17) inalenga kuipa sapoti Timu ya Taifa ya Tanzania, Serengeti Boys, na si kufanya siasa kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakidai.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya safari hiyo, Manara amesema dhamira kubwa ya mashabiki hao ni kuwapa hamasa vijana wa Serengeti Boys ili wasijisikie wapweke wanapokabiliana na Senegal katika mchezo huo muhimu wa fainali.
“Hatuendi Morocco kufanya siasa wala kuingilia majukumu ya timu. Tunakwenda kuishangilia timu yetu ya taifa, kuwapa moyo wachezaji wetu na kuhakikisha wanahisi nguvu ya Watanzania wote waliopo nyuma yao,” amesema Manara.
Alieleza kuwa uwepo wa mashabiki wa Tanzania uwanjani utakuwa chachu ya kuongeza morali kwa vijana hao, hasa wakikabiliana na Senegal ambayo inatarajiwa kuwa na idadi kubwa ya mashabiki wake.
Manara alimshukuru Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha safari hiyo kupitia ndege ya Serikali, akisema hatua hiyo inaonesha uzalendo na dhamira ya dhati ya kuunga mkono maendeleo ya michezo nchini.
Amesema msaada huo utawapa nguvu zaidi wachezaji wa Serengeti Boys katika harakati zao za kutafuta taji la Afrika na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania kimataifa.
Serengeti Boys wanatarajia kushuka dimbani kuikabili Senegal leo katika fainali ya AFCON U-17 huku Watanzania wengi wakisubiri kwa hamu kuona timu hiyo ikiandika historia kwa kutwaa ubingwa wa bara la Afrika.




