Ligi Kuu

Hii ndio sababu Pedro kutimuliwa Yanga

DAR ES SALAAM: OFISA Habari wa Yanga SC, Ally Kamwe amefafanua sababu za uongozi wa klabu hiyo kufanya uamuzi wa kuachana na Kocha Mkuu Pedro Gonçalves, akibainisha kuwa uamuzi huo haukutokana na matokeo ya uwanjani pekee, bali tathmini ya kina ya mwenendo wa timu.

Yanga ilitangaza kuachana na Pedro Jana baada ya kumalizika kwa mechi dhidi ya KMC waliyoibuka na ushindi wa bao 1-0. Mashabiki walimzoea Kocha huyo kwenye mechi hiyo kuonesha kutoridhishwa na mwenendo.

Kamwe amesema uongozi ulifanya tathmini pana ikihusisha si tu idadi ya pointi au mabao, bali pia kiwango cha uchezaji na namna timu inavyopata ushindi.

“Uongozi ulifanya tathmini sio matokeo peke yake wala idadi ya pointi wala sio idadi ya magoli ya kufunga na kufungwa,” amesema Kamwe.

Ameongeza kuwa Yanga kama klabu kubwa huangalia mambo mengi zaidi ikiwemo mfumo wa uchezaji, uongozi wa timu na kiwango cha jumla cha kiufundi.

“Tunashinda lakini tunashindaje? Timu kama Yanga inakusanya vitu vingi. Kuna uongozi wa timu na kiwango cha timu. Tunashinda mechi lakini tunatafuta namna ya ushindi,” alifafanua.

Kamwe amesema tathmini hiyo imebaini kuwa timu haikuonesha kiwango kilichotarajiwa na viongozi pamoja na mashabiki.

“Tumefanya tathmini tumegundua timu haina mwenendo mzuri. Kila mwanayanga aliyekuwa akitazama kiwango cha timu aliona hatuchezi katika kiwango kinachofikiriwa,” amesema.

Ameongeza kwa utani kuwa hata ushindi wa timu hiyo umechangia presha kwa wapinzani, akirejea kauli kwamba “furaha ya watani wetu imetoka kipindi cha hivi karibuni.”

Kwa sasa, Yanga SC imeweka uongozi wa benchi la ufundi chini ya makocha Patrick Mabedi na Abdihamid Moallin, huku Mathew Silva akiwasaidia katika majukumu ya kiufundi.

Uongozi wa Yanga umeeleza kuwa maamuzi yaliyofanyika yanalenga maslahi mapana ya klabu, huku lengo kuu likiwa ni kufikia mafanikio mwishoni mwa msimu.

“Haijalishi tuna makocha wangapi, mwisho wa msimu tunapata nini ndio malengo yetu,” amesema Kamwe.

Wakati huo huo, Yanga inaendelea na maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya Coastal Union utakaochezwa Jumamosi, huku ikiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu yao uwanjani.

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button