Nyumbani

Serikali yaidhinisha katiba mpya ya Simba

Yawabeba wanachama

DAR ES SALAAM: SERIKALI kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) imetangaza rasmi kuidhinishwa kwa marekebisho ya Katiba ya Klabu ya Simba Sports Club, hatua inayohitimisha mchakato wa muda mrefu wa mageuzi ya uendeshaji wa klabu hiyo na kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji huku ikilinda maslahi ya wanachama.

Akizungumza na Waandishi wa habari Dar es Salaam leo Februari 18, 2026 Msajili wa Vyama vya Michezo Abel Ngilangwa, amesema amekamilisha jukumu hilo kufuatia maelekezo ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, aliyemtaka kuhakikisha mchakato huo unahitimishwa kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Amesema hatua iliyokuwa imebaki ilikuwa ni kukabidhi Katiba iliyoidhinishwa kwa uongozi wa klabu na kusaini nyaraka za kukubaliana na marekebisho hayo, jambo ambalo sasa limekamilika kwa mujibu wa sheria na kanuni za usajili wa vyama vya michezo.

Ngilangwa alifafanua kuwa Simba ilianza mageuzi ya mfumo wa uendeshaji kwa lengo la kuruhusu uwekezaji kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 2018, lakini ilikumbana na changamoto za kisheria na kiutawala ikiwemo muundo wa umiliki, usajili wa wadhamini na uoanifu na matakwa ya taasisi za Serikali.

Amesema marekebisho hayo yalipitishwa na Mkutano Mkuu wa wanachama Novemba 30, 2025 na kuwasilishwa kwa Msajili Desemba 10, 2025 kabla ya kurejeshwa kwa maboresho mara kadhaa hadi toleo la mwisho lililowasilishwa Februari 5, 2026.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 11 ya Kanuni za Msajili wa Vyama vya Michezo (T.S Na. 441 ya mwaka 1999), Serikali ilifanya uchambuzi wa kina wa kisheria na kujiridhisha kuwa marekebisho hayo hayaathiri usalama, amani wala maendeleo ya klabu.

Maboresho yaliyoidhinishwa ni pamoja na: Kuanzishwa kwa kampuni ya Simba Sports Club Company Limited itakayoshughulikia shughuli za kibiashara na kiutendaji.

Hisa za klabu kumilikiwa kupitia Baraza la Wadhamini kwa niaba ya wanachama.
Kuimarishwa kwa Baraza la Wadhamini lenye wajumbe kati ya watano hadi saba.

Mkutano Mkuu kubaki kuwa chombo chenye mamlaka ya mwisho ya uteuzi na uondoaji wa wadhamini.Wanachama kubaki na angalau asilimia 51 ya hisa kwa mujibu wa sheria.

Amesisitiza kuwa muundo huo hauanzishi mfumo mpya bali unatekeleza uwiano wa umiliki uliokwisha pitishwa na wanachama.

Sababu za kuidhinishwa
Ngilangwa amesema idhini hiyo imetolewa kwa kuwa marekebisho hayo yanaendana na Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa, yanaimarisha utawala bora na yamezingatia ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali uliotaka kuwepo kwa kampuni moja ya uendeshaji wa klabu huku mali zisizohamishika zikiendelea kumilikiwa na wanachama kupitia wadhamini.

Ameongeza kuwa mabadiliko hayo yameondoa changamoto za kisheria zilizokuwa zinakwamisha mchakato, hasa kuhusu uoanifu na taasisi kama RITA na FCC, na kuweka msingi imara wa usimamizi wa mali na uwekezaji.

Ngilangwa amesema Serikali haina jukumu la kuamua mfumo wa uendeshaji wa klabu bali kuidhinisha maboresho yanayokidhi matakwa ya sheria baada ya wanachama kufanya maamuzi yao.

Ametoa wito kwa wanachama na wadau wa Simba kuheshimu maamuzi hayo ili klabu iendelee kwa utulivu, mshikamano na mafanikio zaidi.

Related Articles

Back to top button