Silva: Kushindwa Anfield kungeua mbio za ubingwa

MANCHESTER: NAHODHA wa Manchester City, Bernardo Silva, amesema kuwa chochote tofauti na ushindi dhidi ya Liverpool kingeua kabisa matumaini ya timu yake katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England.
Kauli hiyo ilitolewa baada ya kikosi cha Pep Guardiola kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Liverpool katika uwanja wa Anfield.
City walikuwa hatarini kubaki nyuma kwa pointi tisa dhidi ya vinara Arsenal, baada ya Liverpool kupata bao la kuongoza kupitia Dominik Szoboszlai aliyefunga kwa mkwaju wa adhabu wa kuvutia dakika za lala salama.
Hata hivyo, Bernardo Silva aliirejesha City mchezoni kwa kusawazisha dakika ya 84, jambo lililochochea dakika za mwisho zilizojaa vurugu na sintofahamu.
Mshambuliaji Erling Haaland aliifungia City bao la ushindi dakika ya tatu ya muda wa nyongeza, lakini mchezo haukuishia hapo. Kulizuka vurugu na mabishano.
Kipa wa Paris Saint-Germain, Gianluigi Donnarumma, aliyekuwa uwanjani, aliokoa kwa ustadi mkubwa shuti la Alexis Mac Allister, akiizuia Liverpool kupata bao la kusawazisha.
Kwa upande mwingine, Rayan Cherki alidhani amehitimisha ushindi kwa kufunga bao la tatu akiwa mbali na lango baada ya kipa wa Liverpool Alisson Becker kupanda juu kusaka bao la kusawazisha. Hata hivyo, bao hilo lilifutwa baada ya mwamuzi kubaini kuwa Szoboszlai alimvuta Haaland kabla ya mshambuliaji huyo wa Norway kulipiza kisasi kwa kuvuta pia.
Mwamuzi aliamua kumuonesha Szoboszlai kadi nyekundu kwa kosa la kwanza.
Akizungumza baada ya mchezo, Silva alisema:
“Kwa umbali tulionao dhidi ya Arsenal, kuja hapa Anfield ni jambo gumu zaidi katika Ligi Kuu. Kila mchezaji alijua kabla ya mechi kuwa kama tungepoteza, basi mbio za ubingwa zingekuwa zimeisha.”
Aliongeza:“Bado tuna matumaini na tutapambana hadi mwisho. Tunahitaji kuendelea kufanya kazi yetu, kitu ambacho hatujakifanya vizuri mwanzoni mwa mwaka.”
Ushindi huo ni wa kwanza kwa Manchester City kuifunga Liverpool ugenini mbele ya mashabiki tangu mwaka 2003, na pia ni mara ya kwanza tangu 1937 City kuifunga Liverpool mara mbili katika msimu mmoja wa ligi.
Silva alihitimisha kwa kusema:“Nina furaha sana, lakini pointi hizi zina thamani sawa na pointi za mechi nyingine yoyote. Imekuwa mwanzo mgumu wa mwaka kwa sababu hatukufanya kazi yetu vizuri. Tungeweza kuwa karibu zaidi na Arsenal”.




