Mabula atua Misri kuongeza nguvu Stars

CAIRO: KIUNGO mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Tanzania, Alphonce Mabula, amewasili nchini Misri kuungana na wenzake wa Taifa Stars kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Mabula anajiunga na kikosi hicho akiwa katika kiwango kizuri, baada ya kuifungia bao timu yake ya FC Shamakhi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Azerbaijan, ambapo walipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Zire FC.
Bao hilo limeendelea kuonesha mchango mkubwa wa mchezaji huyo katika kikosi chake pamoja na uimara wa kiwango chake kuelekea michuano mikubwa ya kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kambi ya Taifa Stars, uwepo wa Mabula unatarajiwa kuongeza ushindani ndani ya kikosi, hasa katika eneo la kiungo na mashambulizi, huku kocha Miguel Gamondi akiendelea kuimarisha timu kwa lengo la kupata matokeo chanya AFCON.
Taifa Stars inaendelea na maandalizi nchini Misri, ikilenga kujenga uimara wa kikosi, kuimarisha muunganiko wa wachezaji na kuongeza makali ya ushindani kabla ya kuanza kwa michuano hiyo, ambapo Tanzania itakutana na wapinzani wakubwa barani Afrika.
Mashabiki wa soka nchini wana matumaini makubwa kuona mchango wa Mabula pamoja na wachezaji wengine wa kulipwa nje ya nchi, wakitumia uzoefu wao kuipa Taifa Stars sura mpya na ushindani wa hali ya juu.




