Sakata la Ronaldo latua FIFA

GENEVA: GWIJI wa soka Duniani Cristiano Ronaldo huenda akasubiri takriban wiki tatu kujua urefu wa adhabu yake ya kufungiwa na FIFA kuelekea Kombe la Dunia 2026.
Nyota huyo wa kimataifa Ureno anaweza kufungiwa mechi mbili au tatu kufuatia kadi nyekundu aliyooneshwa Alhamisi baada ya kumpiga kiwiko beki wa Ireland, Dara O’Shea, katika kipigo cha 2-0 jijini Dublin.
Kwa kawaida, FIFA huchukua wiki tatu baada ya raundi za mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026 kutangaza orodha ya adhabu za kinidhamu duniani kote, zikiwemo kadi nyekundu na matukio ya vurugu za mashabiki.

Kwa sasa hakuna shinikizo kubwa kwa FIFA kuharakisha maamuzi, kwani mechi za playoff zitapigwa mwezi Machi mwakani, lakini shauku kuhusu hatma ya Ronaldo ni kubwa. FIFA ilikataa kueleza muda utakaotumika kushughulikia kesi hiyo.
Adhabu ya kutumikia mechi moja ni ya lazima, na Ronaldo atawaachia wenzake Jumapili wakati vinara wa kundi Ureno watakapowakaribisha Armenia walioko mkiani. Ushindi utawafikisha moja kwa moja kwenye fainali zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico




