“Hatufurahii kucheza mechi za LaLiga Marekani” – Flick

BARCELONA: KOCHA wa FC Barcelona, Hansi Flick, amesema yeye na wachezaji wake hawafurahii uamuzi wa La Liga wa kuwalazimisha kusafiri umbali wa takribani kilomita 7,200 kwenda kucheza mchezo wa kawaida wa Ligi nchini Marekani mwezi Desemba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo Ijumaa, Flick alieleza wazi kutoridhishwa na mpango wa kuupeleka mchezo huo wa tarehe 20 Desemba kuchezwa katika Uwanja wa Hard Rock, uliopo Miami Gardens, nyumbani kwa timu ya NFL, Miami Dolphins.
“Wachezaji wangu hawajafurahia, nami pia sijafurahia, lakini La Liga imeamua tukacheze mchezo huo.” – amesema Flick
Awali Rais wa Barcelona, Joan Laporta, alitetea hatua hiyo akisema inalenga kupanua soko la La Liga nchini Marekani na kuongeza mashabiki wa soka la Uhispania katika bara hilo lililotawaliwa na mpira wa kikapu.
Hata hivyo, Flick na wachezaji wake wanaona safari hiyo ni mzigo mkubwa, hasa ikizingatiwa kuwa itafanyika kabla ya mapumziko mafupi ya msimu wa majira ya baridi, huku Barcelona pia ikitarajiwa kusafiri tena kuelekea Saudi Arabia kushiriki Super Cup ya Hispania Januari 7.
Kiungo wa Barcelona, Frenkie de Jong, ameikosoa ratiba hiyo akisema wachezaji tayari wanakabiliwa na michezo mingi na safari za mara kwa mara ambazo zinachosha mwili na akili. Kama ilivyo kwa Barcelona, wapinzani wao Villarreal nao wanashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, jambo linaloongeza utata wa uamuzi huo.
Rais wa La Liga, Javier Tebas, amesema mpango huo wa kupeleka michezo ya ligi nje ya Hispania utakuwa tukio la kila mwaka, huku akifichua kuwa ligi hiyo itatumia ndege maalum kuwasafirisha mashabiki 2,000 hadi 3,000 kutoka Villarreal kwenda Florida kushuhudia mchezo huo.
Barcelona itashuka dimbani Jumamosi hii kuivaa Girona katika mchezo wa La Liga kabla ya maandalizi ya safari hiyo yenye utata.