Odegaard apata majeraha ya goti, kokosa mechi kadhaa

LONDON: KOCHA wa Arsenal Mikel Arteta amesema nahodha wa klabu hiyo Martin Odegaard, atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa wiki kadhaa kutokana na jeraha la goti, wakati huu vinara hao wa Ligi Kuu ya England wakirejea kutoka mapumziko ya michezo ya kimataifa wakiwa na wachezaji kadhaa wanaokabiliwa na majeraha.
Odegaard, ambaye alikosa mechi kadhaa mwezi uliopita kutokana na jeraha la bega, sasa anaungana na wachezaji wengine watatu wa Arsenal walioumia magoti ambao ni washambuliaji Gabriel Jesus, Kai Havertz, na winga Noni Madueke.
“Tutamkosa kwa wiki chache, bado hakuna tarehe rasmi ya kurejea kwake. Lakini anaendelea vizuri. Ni bahati mbaya sana kinachomtokea. Nadhani atarejea baada ya wiki chache, lakini tutasubiri kuona maendeleo yake na jinsi atakavyojisikia. Ni mapema mno kupata jibu la uhakika,” – Arteta aliwaambia waandishi wa habari kuelekea mchezo wa Fulham Jumamosi.
Arsenal watakuwa na kibarua cha kutanua uongozi wao kileleni mbele ya Fulham watakaokuwa nyumbani Craven Cottage kuanzia saa 1:30 jioni. Vijana hao wa Marco Silva wanawavaa Arsenal wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya aston villa na Bournemouth.