Bondia Rahim atamba hakuna anayemuweza

DAR ES SALAAM: BONDIA chipukizi Rahim Omar amewapa changamoto mabondia waliopo kwenye uzani wake na kuwaita kupambana nao ikiwa wanajiona wao ni bora zaidi yake.
“Mimi ni bondia wa uzito wa light middle. Ukidai wewe ni namba moja Tanzania, lakini hujacheza na mimi hujathibitisha chochote,”amesema Omar katika mazungumzo na gazeti hili.
Aliendelea kwa kusema:“Niko tayari kupigana na yeyote. Na siogopi. Nataka kuonesha kwamba vijana wa Tanzania wanaweza,”.
Amesema kwa upande wake na vijana wenzake wanaokuja kwa kasi, wanatarajia mambo makubwa, wana ndoto na malengo wakiami iwapo watapewa nafasi, wataonesha uwezo wao.
Amesema kuwa changamoto kubwa kwa sasa ni ukosefu wa wadhamini na fursa kwa mabondia wachanga:“Promota ni wachache. Wengi wao wanaangalia majina makubwa tu. Kijana mdogo hana nafasi. Lakini sisi tunahitaji sapoti kama walivyopata mabondia wakubwa waliotutangulia.”
Rahim ametumia nafasi hiyo kuwaomba wawekezaji na wadhamini kuingiza fedha zao katika mchezo wa ngumi, akisema:“Ngumi ni biashara. Sio tu kipaji. Kijana anaweza kuwasilisha bidhaa ya biashara kupitia mchezo huu. Tuna mashabiki halisi, watu wa mtaani ambao wako karibu sana na jamii – tofauti na baadhi ya mitandao ya kijamii.”
Rahim amesema wanahitaji jukwaa. Na jukwaa hilo linaweza kutolewa na serikali, mashirika binafsi, na wadau wa michezo.




