Tanzania upande huu ni ya moto

TIMU ya mchezo wa kuogelea ya Tanzania (HPT) imefanikiwa kushinda medali za fedha 3 na dhahabu 10 kutoka kwenye mashindano ya kimataifa ya kuogelea ya nchini Kenya ( Kenya Aquatics National Swimming Championships 2024) kwa mita 50.
Timu hiyo ya HPT ipo nchini humo kuiwakilisha Tanzania baada ya kualikwa kwenye mashindano hayo yaliyoanza kuchezwa jana na leo kutamatika.
Akizungumza na Spotileo, Meneja wa timu hiyo, Francisca Binamungu amesema timu imeondoka na wachezaji wanne, wavulana watatu ambao ni Delbert Kenemo , Mark Tibazarwa na Romeo-Mihaly Mwaipasi na msichana Crissa Dillip.
“Mchezaji Mark ameogelea mbio tano, na kati ya hizo, mbili amepata medali za dhahabu, na medali za fedha tatu naye Romeo ameshindana kwenye mbio tatu, na zote tatu amepata medali za dhahabu, “amesema Francisca.
Amesema muogeleaji wa nne ni msichana Crissa ambaye ameogelea mbio tano na kufanikiwa kupata medali za dhahabu zote tano.
“Leo tunamalizia, mchezaji Delbert ana mbio mbili, Mark ana mbio tatu, Romeo ana mbio tano na Crissa ana mbio tatu, tunatarajia kuendelea kufanya vizuri kwa kuipeperusha Bendera ya Tanzania,” amesema.