Simba, Singida Black Stars nani kumfuata Yanga Fainali?

DAR ES SALAAM:MCHEZO wa pili wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB unatarajiwa kuwa wa kusisimua, ambapo wababe wa soka nchini Simba watavaana na Singida Black Stars Mei 31 kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, mkoani Manyara.
Mchezo huo umekuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka, hasa ikizingatiwa kuwa mshindi wa pambano hilo atapata tiketi ya kuivaa Yanga katika hatua ya fainali.
Yanga tayari imeshafuzu baada ya kuifunga Azam FC kwa mikwaju ya penalti 4-2, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 na muda wa nyongeza.
Simba imefuzu nusu fainali baada ya kuichapa Tabora United mabao 2-0, katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Kwa upande wa Singida Black Stars, waliitoa Mashujaa FC kwa ushindi wa bao 1-0, wakionesha dhamira ya wazi ya kutaka kufika mbali kwenye mashindano haya.
Timu zote mbili zina kiu kubwa ya mafanikio. Simba SC, ikiwa na historia ya mafanikio makubwa kwenye soka la Tanzania, inatafuta kurejesha heshima yake baada ya kupoteza matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.
Kwa upande mwingine, Singida Black Stars wanatafuta nafasi ya kuandika historia kwa mara ya kwanza kwa kufika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho.
Mchezo huu unatarajiwa kuwa wa ushindani mkubwa, ukizingatia kuwa mshindi si tu atapata nafasi ya kumenyana na Yanga kwenye fainali, bali pia atakuwa katika nafasi ya kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa msimu ujao.