La Liga

Flick: Ushindi Copa del Rey ni hamasa

BARCELONA:KOCHA wa vinara wa Laliga FC Barcelona amesema ushindi walioupata wikiendi iliyopita dhidi ya mahasimu wao wakuu Real Madrid na kutwaa kombe la Mfalme (Copa del Rey) unawahamasisha zaidi watakapokuwa nyumbani kuwavaa Inter Milan katika nusu fainali ya Ligi Ya Mabingwa barani Ulaya kesho Jumatano na si kuwapumbaza kama wengi wanavyodhani

Flick ameyasema hayo alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kujua kocha huyo atatumia mbinu gani kuzima furaha iliyojaa katika mioyo ya wachezaji wake baada ya kutwaa kombe hilo hasa kupitia kwenye mchezo wa El Classico.

“Hapana, ninachoona ni kila mtu ‘amefocus’ kwenye mechi hii (mechi dhidi ya Inter) kila mtu anajua ni muhimu kiasi gani kufika kwenye hatua ya fainali ya Champions League. Ushindi dhidi ya Real Madrid ni muhimu sana kuweka morali chanya kikosini” Flick alijibu

“Kushinda El classico ni hamasa na msukumo mkubwa. Tunajua ni vigumu kiasi gani kufikia fainali, ni ndoto ya kila mtu kuwa hapa kwa hiyo ni lazima ‘tufocus’. Tunajua Inter ina baadhi ya wachezaji walio katika umri ambao pengine ni fursa ya mwisho, sina shaka watajitoa kwa 100% kufika fainali. – aliongeza

Inter Milan wapo jijini Barcelona tayari kuwavaa wenyeji wao katika mchezo utaokuwa na vuta nikuvute utakaopigwa katika uga wa Olympic Lluis Companys majira ya saa 4 usiku Afrika Mashariki.

Related Articles

Back to top button