Ligi Kuu

Unaambiwa huyo Mzize balaa linakuja

DAR ES SALAAM: KATIKA hekaheka za Ligi Kuu Tanzania Bara, nyota wa Yanga, Clement Mzize, ameendelea kuwa gumzo baada ya kuongoza mbio za kuwania kiatu cha dhahabu kwa mabao 13.

Hii ni baada ya Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, kueleza kwa kujiamini kuwa mshambuliaji huyo kijana ataendelea kuvunja rekodi hadi mwisho wa msimu.

Kwa mujibu wa Kamwe, mafanikio ya Mzize si ya kubahatisha, bali ni zao la ushirikiano mzuri katika safu ya ushambuliaji ya Yanga. Amewataja wachezaji kama Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua, na hata Price Dube kama nyota wanaosaidia kwa kutoa pasi za mwisho, jambo ambalo linamuwezesha Mzize kutikisa nyavu mara kwa mara.

“Huu sio mwisho wa Mzize kufunga, kwa ubora alionao na namna timu inavyocheza kwa kushirikiana, ni wazi ataendelea kuwa mwiba kwa walinzi wa timu pinzani. Wachezaji wetu hawana uchoyo, kila mmoja anataka kuona timu inapata ushindi” amesema.

Kwa sasa, Mzize anawania kiatu cha dhahabu akiwa mbele ya Jean Ahoua wa Simba (mabao 12) sawia Price Dube huku Jonathan Sowah wa Singida Black Stars akiwa na (mabao 11). Kamwe ameongeza kuwa lengo la Yanga msimu huu si tu kutetea ubingwa wa Ligi Kuu na kutwaa Kombe la Shirikisho la CRDB, bali pia kupeleka mfungaji bora kwa mara nyingine.

“Hatutaki kuacha kitu msimu huu. Tutachukua kila taji, na hata kiatu cha dhahabu kinapaswa kubaki Yanga,” amesema Ofisa huyo wa Yanga ambayo kwa sasa ipo Viswani Pemba kwa ajili ya mashindano ya kombe la Muungano linalooanza kutimua vumbi Alhamisi Aprili 24 na 25 Yanga wanashuka dimba dhidi ya KVZ FC.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button