AFCONAfrica

AFCON 2027 Ni zaidi ya soka

NDOTO ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2027)
zimetimia baada ya Jumatano wiki hii kutangazwa kuibuka na ushindi.

Sasa Tanzania itakuwa mwenyeji wa michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya timu ya taifa Afrika. Tanzania haiko peke yake kwenye uenyeji huo, bali itashirikiana na washirika wake wa ukanda wa Afrika Mashariki ambao ni Kenya na Uganda.

Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe alisema ana matarajio kuwa fainali hizo zitafana. Tanzania ilishaandaa fainali za michuano hiyo kwa vijana, mwaka 2019 bila
shaka inafahamu hekaheka na mikikimikiki yake.

Zile shangwe zilizoonekana kwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro pamoja na mawaziri wenzake wa michezo kutoka Uganda na Kenya, zilitosha kuona furaha waliyonayo wanamichezo wa Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.

Shangwe za Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia ambaye alidondosha chozi la furaha, zinaakisi ni kwa namna gani jambo hilo lilihitajika na bila shaka ni wakati sahihi kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa michuano hiyo.

Rais wa zamani wa TFF, Leodegar Tenga ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) alikuwepo kushuhudia Tanzania na jirani zake wakitangazwa kushinda tenda hiyo, tabasamu lake lilidhihirisha furaha aliyonayo.

Bila kumsahau Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, ambaye ni mwanasoka wa siku nyingi, Ally Mayay na Katibu wa BMT, Neema Msitha waliolipuka shangwe.

Kwenye mitandao ya kijamii Watanzania wamekuwa wakitamba tangu kutangazwa kwa tukio hilo, status za juzi kwenye Whatsapp karibu kila mmoja alipamba na ujumbe wa Tanzania, Kenya na Uganda kuandaa Afcon 2027.

Ushindi huo una maana kubwa kwa wananchi wa Tanzania na Afrika Mashariki mpaka Kati kwa ujumla. Kuwa mwenyeji wa michuano hiyo ni historia kubwa kwani mbali na kuwa mwenyeji lakini Tanzania inakwenda kufuzu kwa mara nyingine tena fainali hizo sababu mwenyeji hufuzu moja kwa moja.

Mpaka sasa Tanzania imefuzu mara tatu fainali hizo ikiwa ni pamoja na mwaka 1980, 2019 na 2023 zitakazofanyika Ivory Coast Januari na Februari mwakani. Kabla ya Fainali za 2027, kutakuwa na fainali za Morocco 2025, sio mbaya jitihada zikafanywa pia Tanzania
ifuzu fainali hizo na kuwa utaratibu wa kudumu.

Haya ni mabadiliko na hatua kubwa katika soka, kutoka kwenye kushiriki fainali za kwanza mwaka 1980 mpaka kuwa mwenyeji, ni maendeleo makubwa.

Ilichukua miaka 40 kufuzu fainali za pili mwaka 2019, lakini sasa hali imeanza kuzoeleka na mwakani Tanzania imefuzu tena, kana kwamba haitoshi mwaka 2027 fainali za michuano hiyo zitachezwa kwenye ardhi ya Tanzania.

Fainali za mwaka 2019 ugeni ulikuwa mwingi, natarajia fainali za Ivory Coast mwakani uenyeji wa michuano hiyo utakuwepo na bila shaka mwaka 2027 lipo jambo ambalo Tanzania inaweza kutoka nalo kwenye michuano hiyo mbali na kutengeneza uchumi.

Baada ya Motsepe kutangaza wenyeji wa 2027, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa shukrani kwa Mungu lakini pia akaagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuandaa viwanja mapema.

“Nawaagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuhakikisha tunafanya maandalizi mazuri ikiwemo kukamilika kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu viwanja viwili vipya vya
kisasa vya michezo Arusha na Dodoma,” alisema Rais Samia kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X.

Ndio, ni wakati wa Wizara husika kukamilisha hilo ili ikiwezekana kuvutia Caf mechi ya fainali ichezwe kwenye moja ya viwanja vya Tanzania. Wakati ni huu kuanza kutengeneza miundombinu, hoteli na sehemu mbalimbali za burudani ili kuwa tayari kwa michuano hiyo.

Na hapo ndipo sekta binafsi zinapotakiwa kuchangamkia fursa ya kujenga mahoteli makubwa ya kitalii kama ilivyo ndoto za Rais Samia. Hili ni suala la kitaifa na Afrika Mashariki kwa ujumla, isiachiwe serikali na TFF pekee, kuwe na umoja wa kufanikisha hilo na michuano iwe ya mafanikio kama anavyotamani rais wa Caf.

Faida ni nyingi michuano kufanyika Afrika Mashariki ukiondoa kuimarika na kufahamika kwa ligi za nchi hizo, lakini wageni wengi watafika na pia wazawa watapata ajira za muda mfupi.

Wafanyabiashara kama wa vyakula, benki, wachuuzi wa vitu mbalimbali utakuwa wakati wao wa kupata ajira na kukuza uchumi wa nchi. Ukiachana na faida za kukuza uchumi, utalii faida nyingine ya michuano hii ni kubaki na miundombinu itakapokamilika.

Barabara zitaendelea kutumiwa na Watanzania, viwanja vitaendelea kutumika lakini pia wanamichezo watapata nafasi ya kuonana na wachezaji wakubwa Afrika na duniani sababu
wapo Waafrika wanaocheza kwenye ligi kubwa duniani.

Aidha, ni wakati wa wachezaji kuonesha uwezo na vipaji vyao sababu kwenye michuano hii pia wanakuja mawakala kutafuta wachezaji kwani dunia inafuatilia michuano hii. Jambo lingine ambalo wana Afrika Mashariki hawatajuta kuwa wenyeji wa michuano hii ni namna
itakavyozidisha umoja na mshikamano.

Yapo mambo mengi yamefanyika kwa kushirikiana katika nchi hizi, na bila shaka Afcon itakuwa mwendelezo wa yale mazuri yaliyopita. Michuano hii itadhihirisha undugu uliopo kwa nchi hizo na hii ni kwa nchi zote zilizopo kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kati
(EAC).

Ni kazi ya nchi hizo kuendelea kuimarisha amani iliyopo ili isije kutia doa kwa wageni watakaofika kwenye michuano hiyo. Wakati ni sasa, umoja, mshikamano uimarishwe.

Related Articles

Back to top button