2Face ataka kuonana na Alikiba Mbeya

DAR ES SALAAM:MSANII mkongwe wa muziki kutoka Nigeria, Innocent Idibia ‘2Face’, ametaka kuonana na mwanamuziki nyota wa Tanzania, Ali Kiba, atakapokuwa nchini kwa ajili ya kutumbuiza katika maadhimisho ya miaka 30 ya muziki wa Bongo Fleva yatakayofanyika mkoani Mbeya Jumamosi hii.
Akizungumza kuelekea tamasha hilo, mmoja wa waandaaji wa maadhimisho hayo, Hamadi Ally Seneda maarufu Madee, amesema 2Face ameonesha nia ya kukutana na Ali Kiba, lakini juhudi za kuwasiliana na msanii huyo wa Tanzania zimebaini kuwa ana ratiba nyingine.
Madee amesema walimtafuta Ali Kiba ili kufahamu uwezekano wa kukutana na 2Face, lakini walielezwa kuwa msanii huyo ana majukumu mengine yaliyomfanya ashindwe kupata nafasi kwa wakati huo.
“2Face ameulizia kukutana na Ali Kiba. Tulimcheki Ali Kiba, akasema ana ratiba nyingine, watajitahidi kumkutanisha nae akifika Dar wataonana Kiba ataweza kwenda Mbeya” amesema Madee.
Ameongeza kuwa 2Face atakuwa na ratiba yake ya shughuli atakapowasili Mbeya, huku uwezekano wa kukutana na Ali Kiba ukitegemea upatikanaji wa muda kwa pande zote mbili.
2Face anatarajiwa kuwa miongoni mwa wasanii watakaopanda jukwaani katika maadhimisho ya miaka 30 ya Bongo Fleva yatakayofanyika Mbeya Jumamosi hii, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha safari ya muziki huo na mchango wake katika tasnia ya burudani nchini.




