Amani yatawala familia ya Rayvany, Marioo

DAR ES SALAAM: BAADA ya juhudi za Msanii wa Bongo Fleva, Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’, kuwakutanisha Fahyma na Paula Paul, dalili za maridhiano zinaendelea kuonekana huku amani ikitawala kati ya familia ya Rayvanny na Marioo.
Hatua hiyo imeonekana wazi baada ya Paula kutumia mitandao ya kijamii kumchapisha picha ya Jaydan, mtoto wa Fahyma na Rayvanny, na kuandika ujumbe uliovutia wengi akisema angetamani mtoto huyo aje kuwa mkwe wake siku zijazo.
Akijibu ujumbe huo kwa utani na ishara ya kuonyesha kuwa tofauti zilizokuwepo zimekwisha, Fahyma ameandika, “Imeisha hiyo,” kauli iliyopokelewa vyema na mashabiki wao waliofurahia kuona uhusiano mzuri ukirejea kati ya pande hizo mbili.
Katika tukio jingine lililozua gumzo mitandaoni siku hiyo hiyo, Jaydan alikutana kwa mara ya kwanza uso kwa uso na msanii Marioo.
Wawili hao walipata nafasi ya kupiga picha za pamoja, jambo lililozidi kuonyesha kuwa sasa kuna hali ya ukaribu na maelewano kati ya familia hizo.
Mashabiki wengi wameendelea kupongeza hatua hiyo, wakieleza kuwa maridhiano na upendo kati ya familia za wasanii ni mfano mzuri kwa jamii na huchangia kujenga mazingira bora ndani ya tasnia ya burudani nchini.




