Mwambusi apewa mfupa uliomshinda Ouma

ARUSHA: UONGOZI wa Coastal Union umemtangaza Juma Mwambusi kuwa mkuu wa benchi la ufundi la timu hiyo akichukuwa mikoba ya David Ouma aliyefutwa kazi mapema msimu huu.
Kwa mujibu wa Ofisa habari wa Coastal Union, Abass Elsabri amesema Mwambusi atashirikiana na kocha msaidizi, Joseph Lazaro kukinoa kikosi cha timu katika michezo yote ya ligi kuu.
“Ubora, weledi, mipango, mikakati na uwezo wako kila Mtanzania anaujua, sasa malengo yetu ya kumaliza moja kati ya nafasi nne za juu yanakwenda kutimia kwa asilimia 100.
Anaifahamu Ligi ya Tanzania na amewahi kufundisha klabu kubwa na kongwe hapa nchini, wanamangushi wanajua uwezo wako na ari yako ya kupambania alama 3 kwa kila mchezo,” amesema Abass.
Mwambusi aliyewahi kuwa kocha msaidizi wa Yanga miaka kadhaa iliyopita amekabidhiwa Coastal Union na mechi inayofuata ni dhidi ya Yanga, mchezo utakaochezwa Oktoba 26, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.