Zuchu: Ng’ombe ndiye role model wangu!

DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva, Zuhura Othuman ‘Zuchu’, amezua gumzo mitandaoni baada ya kumjibu shabiki aliyemkosoa kuhusu uamuzi wake wa kuvaa kipini puani, akidai mapambo hayo yanamfanya aonekane kama ng’ombe.
Mjadala huo uliibuka katika mtandao wa Instagram, baada ya shabiki huyo kumweleza Zuchu kuwa kipini alichovaa puani hakimpendezi na kumshauri kurejea katika uvaaji wa kipini cha dhahabu akidai unampa mwonekano wa kuvutia zaidi.
Katika maoni yake, shabiki huyo aliandika kuwa mapambo hayo yanafanana na yale yanayovaliwa na ng’ombe wa Kimasai, huku akimshauri msanii huyo kujipenda na kuzingatia mwonekano wake.
Hata hivyo, Zuchu hakukubaliana na ukosoaji huo, badala yake alimjibu shabiki huyo kwa maneno yaliyozua mjadala zaidi, akisema anapenda uchafu na kwamba ng’ombe ndiye anayemchukulia kama mfano wa kuigwa (role model).
“Napenda uchafu, Isabela. Na ng’ombe ndiye role model wangu,” alijibu Zuchu.
Majibizano hayo yamevutia hisia za watumiaji wa mitandao ya kijamii, huku baadhi wakiona ni namna ya msanii huyo kuonyesha kuwa yuko huru kufanya maamuzi kuhusu mwonekano wake bila kuyumbishwa na maoni ya watu.
Kwa upande mwingine, tukio hilo limeongeza gumzo kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii na namna mastaa wanavyokabiliana na ukosoaji kutoka kwa mashabiki wao, hasa pale maoni yanapogusa mwonekano na mitindo yao ya mavazi.
Zuchu ni miongoni mwa wasanii wa kike wanaovutia mijadala katika tasnia ya Bongo Fleva, si kwa muziki wake pekee, bali pia kwa mitindo yake na matukio mbalimbali yanayojadiliwa mitandaoni.




