Yanga yazitaka tatu za TP Mazembe

LUBUMBASHI: KIKOSI cha Yanga kitashuka dimbani kesho kusaka alama tatu muhimu katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.
Kuelekea mchezo huo Kocha wa Yanga, Sead Ramovic amesema malengo yao ni kuonesha uwezo wao na kufanya vizuri kesho.
Ramovic amesema haijalishi wapinzani wao wako vipi , wanafahamu TP Mazembe ni timu kubwa, ina wachezaji wazuri, kesho mashabiki na wanasoka watashuhudia mechi nzuri.
“Nafahamu kuwa mchezo wa mwisho hapa Congo Yanga ilishinda lakini hatuwezi kuzungumzia yaliyopita, tunautazama mchezo wa Mazembe kama mpya na tupo tayari kwa changamoto hii,” amesema.
Ramovic amesema jambo kubwa mashabiki wa Yanga wamelifanya, kusafiri kwa bus kutoka Dar es salaam mpaka Lubumbashi jambo hilo sio rahisi.
“Ni Faraja kwetu na inatupa motisha ya kuwa tuna watu wanaotupa moyo, kutufanya tusiyumbe, kwa kweli nachoweza kusema ni kwamba tupo hapa kuwapa furaha timu nzima inatambua umuhimu wa mashabiki wetu, tutapambana kuhakikisha tunawafurahisha wananchi,”.
Mwakilishi wa wachezaji wa Yanga, Max Nzengeli amesema wanashukuru Mungu wamefika salama na wapo Lubumbashi kwa ajili ya kupambana.
“Kweli hatujashinda mechi zetu za mwanzo lakini haimaanishi tukae vichwa chini, muda huu ni wa kurudi juu na kuwapa furaha wananchi, tunatambua ukubwa wa TP Mazembe, tunapambana kwa ajili ya kushinda kesho
Tunasema Asante kwa mashabiki wa Yanga siyo rahisi kusafiri kwa bus mpaka hapa, haitakuwa rahisi lakini tunawahakikishia tutapambana sana kwa ajili yao Tunashukuru sana kwa kujitoa kwa ajili yetu,” amesema Nzengeli