Yanga yalenga makundi CAFCL

DAR ES SALAAM: Rais wa Yanga Eng. Hersi Said amesema malengo ya mabingwa hao wa soka la Tanzania kimataifa msimu ujao ni kufika hatua ya makundi kwakuwa klabu hiyo kwa sasa haijatangaza vyema jina lake katika Nyanja hiyo
Hersi ameyazungumza hayo katika mahojiano na chombo kimoja cha Habari nchini wakati akitolea ufafanuzi swali lililohusu mipango yake kuhakikisha Yanga inapaa kimataifa kwa msimu ujao wa 2025/2026.
“Kiukweli hatujawa na matokeo mazuri kwenye michuano ya Kimataifa kwa mfululizo miaka ya hivi karibuni kama tuliokuwa nayo hapa ndani, na mashindano ya Afrika ni mashindano ambayo yanahitaji maandalizi makubwa” amesema
“Tulifika fainali Kombe la Shirikisho Afrika, baadae tukafika robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sababu tulikuwa hatujaingia makundi kwa miaka 25 na baadae msimu huu tukaishia Makundi Kwahiyo kwa msimu ujao malengo ya Yanga ni kuingia kwanza kwenye hatua ya makundi, na tukishaingia makundi tutabadilisha upepo hapo.” aliongeza
“Tukishaingia kwa msimu wa tatu mfululizo tunatengeneza malengo mapya, tutafanya usajili ambao ni wa kimalengo na kimkakati na wachezaji watakaokuja kwa sababu watakuwa ni wenye ubora nao hawataishia Makundi”.
Yanga ndio mabingwa wa soka la Tanzania msimu huu wakiwa wametwaa mataji yote ya ndani kwa msimu uliomalizika huku wakiwa wameishia hatua ya makundi ya Ligi ya mabingwa Afrika katika msimu ambao walitarajiwa kufanya makubwa kutokana na ubora wao katika soka hivi sasa.