Africa

Yanga yaja na kampeni “Tutafuzu Nyumbani”

DAR ES SALAAM: KLABU ya Yanga SC imezindua imekuja na kampeni maalum iliyopewa kaulimbiu “Tutafuzu Nyumbani” ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha mashabiki kuelekea mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.

Kampeni hiyo inakuja baada ya Wananchi kupoteza mchezo uliopita ugenini dhidi ya FAR Rabat ya Morocco kwa bao 1-0, matokeo yaliyopunguza kwa kiasi kikubwa nafasi yao ya kufuzu hatua ya robo fainali, isipokuwa kwa kutegemea mahesabu magumu.

Kimahesabu, Yanga imebakiza mchezo mmoja pekee wa kuhitimisha hatua ya makundi, huku hatma yao ikitegemea pia matokeo ya timu nyingine.

Wananchi wanalazimika kushinda kwa tofauti ya angalau mabao mawili dhidi ya JS Kabylie ya Algeria, sambamba na kumuombea Al Ahly ya Misri iwafunge FAR Rabat kwa mabao mawili au zaidi.

Ni hali inayoufanya mchezo huo kuwa mtihani mzito kwa Yanga, lakini pamoja na ugumu uliopo, Msemaji wa klabu hiyo, Ally Kamwe, amesema bado matumaini yapo.

Kamwe amewataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuipa nguvu timu yao katika pambano hilo muhimu, akisisitiza kuwa sapoti ya mashabiki inaweza kuwa silaha kubwa ya kufanikisha ndoto ya kufuzu.

“Jumapili ni siku ya Wananchi. Tunahitaji uwanja uwe wa njano na kijani, mashabiki wajitokeze kwa wingi kuisukuma timu yetu. Bado tunaamini inawezekana,” alisema Kamwe.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button