Yanga waifuata Far Rabat na silaha zote!

DAR ES SALAAM: KLABU ya Yanga inatarajiwa kusafiri leo kuelekea Rabat, Morocco, kwa ajili ya mchezo muhimu wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS FAR Rabat utakaochezwa Jumamosi.
Mchezo huo utakuwa wa tano kwa Yanga katika kundi hilo na ni wa kuamua hatima yao ya kufuzu hatua ya robo fainali, huku wakihitaji matokeo mazuri ili kujiweka katika nafasi nzuri kabla ya kumaliza ratiba ya makundi.
Katika mchezo wa awali uliochezwa Zanzibar kwenye Uwanja wa New Amaan, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS FAR, jambo linalowapa morali ya kuendelea kupambana kwa ushindi au angalau sare wakiwa ugenini.
Wametoka kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly mwishoni mwa wiki na kuendelea kusalia katika nafasi ya pili kwa pointi tano nyuma ya kinara huyo wa Misri yenye pointi nane, huku FAR Rabat ikiwa na pointi tano, na JS Kabylie ya Algeria ikiwa mkiani kwa pointi mbili.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves amesema pambano hilo ni la kufa au kupona kwa timu yake na wanalazimika kucheza kwa juhudi kubwa ili kupata matokeo chanya.
“Mchezo wa AS FAR ni kama fainali kwetu, ni lazima tupambane kwa nguvu zote. Tunajua wapinzani wetu si wa kubezwa, wana kikosi kizuri na watacheza kwa nguvu kubwa wakiwa nyumbani,” amesema Goncalves.
Ameongeza kuwa Yanga itakwenda Morocco kwa tahadhari kubwa huku ikiendelea kuwaheshimu wapinzani wao, lakini lengo kuu likiwa ni kupambana ili kuhakikisha wanapata matokeo yatakayowasogeza hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.




