Africa

Yanga, Simba, Azam, Kipanga ni vita CAF

BAADA ya Geita Gold na KMKM ya Zanzibar kutupwa nje kwenye mechi za awali za michuano ya Afrika, Tanzania sasa tumesaliwa na timu nne zinazowakilisha nchi.

Michuano hiyo inatarajia kuendelea leo na kesho kwa Yanga na Simba kucheza kwenye viwanja tofauti wakiwania kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Azam na Kipanga ya Zanzibar zikipambana kupenya hatua inayofuata ya Kombe la Shirikisho Afrika.

YANGA

Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara baada ya kuifurusha Zalan FC ya Sudan Kusini kwa ushindi wa jumla wa mabao 9-0 kwenye mechi ya hatua ya awali, leo watakuwa na kibarua kingine dhidi ya Al-Hilal ya Sudan kwenye hatua ya pili ya awali.

Hilal inayoongoza Ligi Kuu ya kwao, yenyewe iliitoa St. George ya Ethiopia kwa faida ya bao la ugenini baada ya matokeo ya kufungwa mabao 2-1 ugenini kabla ya ushindi wa nyumbani wa bao 1-0.

Mechi hiyo inatarajiwa kuwa ngumu na ya kuvutia kutokana na ukongwe wa timu hizo na vikosi imara walivyonavyo sasa.

Kingine kinachotia ugumu na hamasa ya mechi hiyo ni kocha wa Hilal, Florent Ibenge raia wa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo ambaye anazifahamu timu za Tanzania akiwa ameshacheza na Simba kwenye michuano hiyo mechi sita katika misimu ya hivi karibuni.

Hata hivyo, kinachowapa moyo Yanga ni hali ya kocha huyo kukosa matokeo kila anapotua kuumana na Simba kwenye ardhi ya Tanzania licha ya vikosi alivyokuwa navyo kuonesha soka safi.

Alikutana na Simba akiwa anainoa AS Vita msimu wa 2018-19 na 2020-21 kabla ya msimu uliopita akiwa na RS Berkane ya Morocco alikutana na Simba hatua ya makundi ambapo alishinda kwao kwa mabao 2-0 na alipotua Tanzania akafungwa bao 1-0.

Yanga inayonolewa na Mtunisia, Nasreddine Nabi imeendeleza makali yake kwenye ligi lakini pia ikitakata katika Ligi ya Mabingwa huku mchezaji tishio anayetajwa mno kwa wapinzani ni Fiston Mayele aliyefunga ‘hat-trick’ mara mbili kwenye mechi mbili za mwisho za michuano hiyo.

Bado vitendawili ni vingi katika mchezo huu kwani Yanga pamoja na kuwa na kikosi kizuri safari hii lakini kushindwa kuingia hatua ya makundi ya michuano tangu mwaka 1998 imezidi kuwapa morali na kuhitaji ushindi leo kabla ya marudiano mnamo Oktoba 16, mwaka huu.

Lakini pia ni mechi itakayokuwa na maswali mengi kwa Ibenge akihitaji kumaliza gundu la kushindwa kupata ushindi Tanzania na pia kutetea kibarua chake kwa kuipelekea makundi timu yake hiyo mpya aliyojiunga nayo msimu huu akitokea Berkane.

SIMBA

Wekundu wa Msimbazi nao watakuwa kibaruani kesho ugenini huko Luanda, Angola wakipepetana na Primeiro de Agosto ya nchini humo.

Simba ambayo iliibamiza Big Bullets ya Malawi kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-0, wanakutana na wababe hao walioitoa Red Arrows ya Zambia kwa ushindi wa mabao 2-1 baada ya mechi mbili.

Simba inakutana na de Agosto ikiwa haina kumbukumbu nzuri dhidi ya timu za Angola baada ya mwaka 2013 kufurushwa nje kwa kufungwa jumla ya mabao 5-0 na Recreativo do Libolo, hivyo leo itakuwa na kibarua cha kufuta rekodi hiyo mbaya na kuweka mpya.

Hata hivyo, mechi hiyo itakuwa kibarua kingine cha kocha wa muda wa Simba, Juma Mgunda ambaye anahitaji kuendeleza rekodi ya Simba ya kucheza makundi na kufika robo fainali kwa misimu minne iliyopita.

Pamoja na hayo, lakini mazingira ya Simba kuanzia ugenini hatua hii na kumalizia nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam inawapa faida ya kujipanga sawa sawa hata kama kutakuwa na matokeo ya tofauti kwenye mchezo wa kesho.

Aidha, wakati de Agosto wakiingia dimbani huku kwenye ligi ya kwao wakiwa nafasi ya tano, Simba wao wataingia wakiwa vinara wa ligi na hasa wakichagizwa na morali ya ushindi wa mabao 3-0 walioupata kwa Dodoma Jiji hivi karibuni.

Kwa vyovyote, Simba itahitaji kupambana na kuvuja jasho mpaka mwisho katika mchezo huo kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ili kuendeleza utamaduni walionao sasa wa kucheza makundi kila msimu wakipigania ndoto yao ya kufika fainali.

AZAM

Azam ambayo yenyewe ilikuwa ikisubiri kuanzia hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho kama ilivyoelekezwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), leo itakuwa dimbani dhidi ya Al Akhdar ya Libya.

Akhdar yenye makazi yake mjini Benghazi ilifika hatua hiyo kwa kuitoa Al- Ahli Khartoum kwa ushindi wa mabao 3-0 ilioupata nyumbani kabla ya kutoka suluhu ugenini.

Azam ambayo haijawahi kushiriki hatua ya makundi ya michuano hiyo, inahitaji kupambana na kuandika rekodi mpya msimu huu kutokana na kariba ya wachezaji walionao katika kikosi chao ambacho msimu huu kimepania kuonesha ushindani mkali.

Majina ya wachezaji kama Tape Edinho, Issa Ndala, Kipre Junior, James Akaminko, Malickou Ndoye, Abdul Sopu na wengine waliotua msimu huu ni miongoni mwa wachezaji wanaoibua matumaini kwa mashabiki wa timu hiyo na hata wanachokifanya wanapokuwa uwanjani.

Mara kadhaa uongozi wa Azam umejinasibu juu ya usajili huo ambao umetawaliwa na picha ya michuano ya Afrika japokuwa kwenye ligi bado wanapata changamoto dhidi ya washindani wao.

Kwa sasa Azam inashikilia nafasi ya nne ikiwa na pointi 11 sawa na Namungo waliopo nafasi ya tatu huku ikizidiwa pointi mbili na vinara Simba na Yanga wanaoshika nafasi mbili za juu.

Kwa lugha ya soka bado hawajafanya vibaya, isipokuwa wanahitaji kuweka mambo sawa ili waendelee kuishi kwenye ndoto yao ya ushindani na mafanikio msimu huu kwenye michuano wanayoshiriki.

Kocha wao mpya, Denis Lavagne anahitaji kuonesha kitu akiwa na kikosi hicho kipana, ubora wake, mbinu na ujuzi alionao ndiyo tegemeo pekee sasa kwa Azam baada ya kufanyika kazi kubwa ya kuunda kikosi chao.

KIPANGA

Wawakilishi pekee waliosalia kutoka Zanzibar, Kipanga wameonesha kazi nzuri baada ya kuitupa nje Al Hilal Wahu ya Sudan Kusini na leo wanakutana na Club Africain ya Tunisia.

Kipanga ambayo iliipiga Wahu kwa penalti 4-3 baada ya sare ya 2-2 ya matokeo ya jumla itakuwa kibaruani kwa kuanzia nyumbani kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Kipanga ambao ni mabingwa wa Kombe la FA msimu uliopita, wanakutana na Africain ambayo inashika nafasi ya saba kwenye Ligi Kuu Tunisia lakini pia hivi karibuni wamekuwa na matokeo ya kusuasua.

Pamoja na hayo lakini Kipanga inapaswa kuwapa heshima wapinzani wao hao kutokana na ukongwe na ukubwa walionao kwenye michuano ya Afrika japokuwa hawana rekodi nzuri pia katika miaka ya hivi karibuni.

Kingine Africain kuanzia kwenye hatua ya pili ya awali ya michuano hiyo ni jibu tosha kwamba Kipanga inapaswa kujipanga kiyakinifu kwa ‘level’ ambayo ipo Africain mpaka inaanzia hatua ya pili na si ya kwanza kama ilivyokuwa kwa Kipanga.

Ni muhimu kwa Kipanga kupambana leo kutafuta matokeo mazuri nyumbani kabla ya kwenda kupigania hatima yao ugenini. Ni wazi kuwa ushindani wa timu za Zanzibar ni tofauti na ushindani wa Ligi ya Tunisia lakini soka halina mwenyewe na huendana na anayeliheshimu.

Kipanga waingie kwa tahadhari na heshima juu ya mpinzani wao wakifahamu mioyoni mwao wanachohitaji ni ushindi mzuri wa nyumbani utakawaobeba ugenini watakapokwenda kupambana kufa au kupona kuendelea kuiweka Zanzibar kwenye ramani ya mashindano hayo msimu huu.

Related Articles

Back to top button