Yanga kazini Leo kuivaa Cosmopolitan

DAR ES SALAAM: MABINGWA watetezi wa Kombe la Shirikisho la CRDB, Yanga, leo wanatarajiwa kushuka dimbani katika Uwanja wa KMC Complex kuanza rasmi kampeni ya kutetea taji hilo kwa kuvaana na Cosmopolitan katika mchezo wa hatua ya 64 bora utakaopigwa saa 1:00 usiku.
Yanga wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na morali ya juu baada ya kuhitimisha hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya JS Kabylie, ushindi uliowapa heshima licha ya kushindwa kufuzu robo fainali.
Kutolewa kwenye michuano ya Afrika kunafanya miamba hiyo ya Jangwani sasa kuelekeza nguvu na akili zao kwenye mashindano ya ndani wakilenga kutetea ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB pamoja na kuendeleza ushindani katika Ligi Kuu.
Kwa upande wa ubora wa vikosi, Yanga wanaonekana kuwa na faida kubwa kutokana na uzoefu, ubora wa wachezaji na benchi la ufundi, lakini historia ya mashindano ya mtoano inaonesha kuwa mechi za aina hii huwa na ushindani mkubwa kwani timu ndogo huingia kwa ari ya ziada kutafuta matokeo ya kushangaza.
Cosmopolitan, mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu msimu wa 1967/68, wanashuka dimbani wakibeba rekodi nzuri kwenye First League wakiwa nafasi ya pili katika kundi lao na pointi 13 baada ya michezo saba, jambo linaloashiria kuwa si wapinzani wa kubezwa.
Motisha kubwa kwao itakuwa ni kupata matokeo chanya dhidi ya mabingwa hao watetezi, huku ikiwa ni fursa kwa wachezaji wao kujitangaza zaidi mbele ya jukwaa kubwa.
Kwa Yanga, ushindi wa leo ni muhimu ili kuanza vizuri safari ya kutetea taji, lakini wanapaswa kuwa makini dhidi ya Cosmopolitan ambao bila shaka wataingia uwanjani kwa tahadhari, nidhamu na presha ndogo.




