
DAR ES SALAAM:MSANII maarufu wa filamu nchini, Jacqueline Wolper, amesema kuwa kwa sasa hawezi tena kushiriki katika kuchapisha picha au maudhui yasiyo na maadili kwenye mitandao ya kijamii, akisema maisha yake yamebadilika na sasa anawaza zaidi kuhusu athari kwa watoto wake.
Wolper amesema kuwa akiwa mama, amekuwa akitathmini kwa kina kila kitu anachokiposti, akihofia namna kitakavyomwathiri yeye binafsi na familia yake, hasa watoto wake wanapokuwa wakubwa.
“Ningekuwa na uwezo wa kubadili yaliyopita, ningeyabadilisha mambo yote mabaya niliyowahi kufanya kipindi cha ujana wangu,” amesema Wolper.
Ameongeza kuwa kwa sasa haoni sababu ya kuendelea kuweka mitandaoni picha au maudhui machafu, kwa sababu anajua watoto wake wanaweza kuyaona au kuathirika nayo hapo baadaye.
“Kwasasa siwezi kabisa kupost mambo machafu kwenye mitandao ya kijamii, nahofia watoto wangu wanakua na wataweza kuona au kuhukumu matendo yangu ya zamani,” amefunguka msanii huyo.
Jacqueline Wolper ni miongoni mwa wasanii waliowahi kuvutia hisia kali mitandaoni kutokana na mtindo wake wa maisha na namna alivyokuwa akijieleza waziwazi.
Hata hivyo, amekuwa mstari wa mbele kuonesha mabadiliko ya maisha na msimamo wake mpya kama mzazi.