Kikapu

Wenye ulemavu kunogesha michuano ya kikapu Ijumaa

DAR ES SALAAM:TIMU za mpira wa Kikapu za wenye ulemavu Ashura na Malilo zinatarajiwa kunogesha michuano ya Kikapu ya Ramadhan inayowahusisha mastaa mbalimbali wa mchezo huo.

Timu hizo zitacheza Ijumaa  Machi 28 kusindikiza nusu fainali mbili za kwanza zikihusisha timu Sudi dhidi ya timu Evans na ya pili itakuwa timu Amini dhidi ya Miyas.

Akizungumza na SpotiLeo Mkurugenzi wa Academia ya Mchenga ambaye ni mmoja ya waandaaji wa michuano hiyo Mohamed Yusufu amesema timu zimeitwa majina ya mastaa wa mchezo huo ili kunogesha na kuvuta mashabiki wengi.

Amesema lengo la michuano hiyo ni kuinua mchezo na vipaji lakini pia, kukusanya fedha zitakazosaidia kununua vifaa vya michezo kwa ajili ya timu za Kikapu za wenye ulemavu.

“Michuano hiyo iliyoanza wiki iliyopita imelenga kukusanya fedha kusaidia timu za wenye ulemavu. Ni michuano iliyobeba majina ya mastaa wakichuana kuwania Kombe la Ramadhan,”amesema.

Amesema shindano hilo ni fursa kwa wachezaji Kikapu kwani wanakutana na kampuni mbalimbali ambazo zikiwaona zinaweza kuwapa ubalozi.

Timu nyingine zitakazonogesha kwenye mechi za utangulizi ni timu All Stars za wanawake kati ya timu Jesca dhidi ya Tukusubira.

Related Articles

Back to top button