Waogeleaji wawili kuondoka Leo kuelekea Singapore

DAR ES SALAAM: WAOGELEAJI wa timu ya Taifa ya kuogelea Collins Saliboko na Michael Joseph wanatarajia kuondoka leo kuelekea Singapore kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Dunia ya Kuogelea huku Baraza la Michezo la Taifa (BMT) likiwakabidhi bendera na kuwatakia kila la heri.
Mashindano ya Dunia ya Kuogelea yanatarajiwa kufanyika nchini Singapore kuanzia Julai 27 hadi Agosti 3, 2025.
Wakati akikabidhi bendera ya Taifa Dar es Salaam kwa nahodha Michael, Ofisa Michezo Mwandamizi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Charles Maguzu amesema hana shaka na uwezo wa waogeleaji hao, anaamini wameandaliwa vizuri kupeperusha bendera ya taifa kimataifa.
Maguzu, amesema mashindano hayo ni fursa nyingine ya kuonesha uwezo mkubwa wa vijana wa Tanzania katika medani za kimataifa.
“Tunatambua kazi kubwa inayofanywa na Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA) katika kukuza mchezo huu na kuitangaza nchi kimataifa. Vijana hawa wameandaliwa vizuri, wana uzoefu na wamewahi kushiriki mashindano ya dunia huko nyuma. Tunaamini wataendelea kupunguza muda wao na kufikia viwango vya kushiriki Olimpiki,” alisema Maguzu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufundi wa TSA, Amina Mfaume, alisema mwaka huu hakuna mwakilishi wa kike kutokana na kutotimia kwa alama za kiufundi zilizowekwa.
“Tulikuwa na kigezo cha pointi 500 kwa waogeleaji wote. Kwa upande wa wasichana waliotimiza vigezo bado ni wadogo kiumri na wanajiandaa kwa mashindano ya dunia ya vijana mwezi ujao, hivyo hawatashiriki haya mashindano ya watu wazima,” alisema Mfaume.
Aliongeza kuwa Saliboko atashiriki mbio za mita 100 freestyle na butterfly, huku Joseph akishiriki mita 50 freestyle na butterfly na kwamba wachezaji Wamepata mafunzo Afrika Kusini na wamejiandaa vizuri.
Naye Mwenyekiti wa TSA, David Mwasyoge alisema anatumai wachezaji watatumia fursa hiyo kuhakikisha wanapunguza muda wao wa mashindano na kujipanga vyema kwa michezo ya Olimpiki ijayo.
Alisema timu hiyo itaongozana na Katibu Mkuu wa TSA kama Meneja wm huku Kocha Mkuu akiwa John Belela, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa TSA.
Nahodha Joseph Michael, alisema wako tayari kuwakilisha nchi kwa heshima na walichonacho ni ari na morali ya kupambana. “Tumejiandaa vizuri, tunaamini tutafanya vizuri na kupunguza muda wetu zaidi. Tunaomba Watanzania watuombee,” alisema.