Muziki

Wanamuziki Congo watunga wimbo kumuenzi Lokassa ya Mbongo

CONGO: WANAMUZIKI wa Congo wakiwemo wapiga gitaa maarufu wa muda mrefu katika tasnia ya muziki wa Congo wataungana na wadau wa muziki kwa ujumla nchini humo kufurahia kumbukumbu ya maisha ya aliyekuwa mpiga gitaa maarufu nchini humo Lokasa ya Mbongo.

Katika kuenzi uwezo wake wapigagitaa wenzake kutoka Congo wametoa wimbo wa heshima. Wimbo huo uliopewa jina la ‘Lokassa Forever’, ulitungwa ili kuenzi kifo cha aliyekuwa kiongozi wa bendi ya Soukous Stars.

Wimbo huo utazinduliwa kwa kushirikiana na mashabiki wa Kinshasa alikokuwa anatoka mwanamuziki huyo na kwingineko siku ya maazimisho ya mwaka wa pili wa kifo chake.

Baadhi ya nyimbo za Lokasa ya Mbongo aliyefariki Machi 2023 na kuzikwa Desemba mwaka huo huo ikiwa ni miezi tisa baada ya kifo chake ni pamoja na ‘Marie’ ‘Jose’, ‘Bonne Anne’, ‘Sophia’, Monica’ na ‘Adiza’.

Katika wimbo huo zinasikika sauti za wagongwe Yondo Sister na Shimita El Dielgo. Wengine walioshiriki kurekodi wimbo huo ni Dally Kimoko aliyepiga gitaa la solo huku Ngouma Lokito akipiga gitaa la bezi.

Akizungumza na Saturday Nation, mwimbaji wa Congo mwenye makazi yake Paris, Ballou Canta amesema wameamua kuuimba upya wimbo wa ‘Monica’ wakiuita ‘Lokassa Forever’ kwa sababu ndiyo wimbo uliopendwa zaidi na Lokasa enzi za uhai wake.

“Tulitaka kumuenzi kwa kutumia mojawapo ya nyimbo zake bora zaidi. Hili tulifanya kwa kuandika upya mashairi na kuanzisha upya wimbo na midundo ya wimbo huo,” Ballou Canta ameeleza.

Kitu cha kufurahisha katika wimbo wa awali Ballou Canta ndiye aliimba sauti kuu kwenye wimbo wa Monica uliotolewa mwaka 1986 na katika wimbo huu yumo.

Baada ya kuacha bendi ya Tabu Ley ya Afrisa International mwishoni mwa 1977, Lokassa alipiga kambi huko Abidjan, Cote d’Ivoire, na miji mingine ya Afrika Magharibi. Baadaye angeishi Ufaransa mwanzoni mwa miaka ya 1980 kabla ya kuhamia Marekani mwishoni mwa miaka ya 1990.

Related Articles

Back to top button