
LIGI Kuu Bara inatarajia kuanza kuunguruma Agosti 15, mwaka huu ikirejea na timu 16 kama ilivyo ada lakini ikiwa na timu mpya tatu; JKT Tanzania, Tabora United na Mashujaa.
JKT Tanzania na Tabora United au zamani Kitayosce zilipanda mapema baada ya kuchuana vizuri kwenye Ligi ya Championship lakini Mashujaa walilazimika kuonesha ushujaa wao mbele ya Mbeya City na kukata tiketi ya kupenya Ligi Kuu.
Timu hiyo inayotoka Kigoma ilicheza mechi mbili za mtoano na Mbeya City kwa mtindo wa mechi za nyumbani na ugenini ambapo mechi ya kwanza walishinda mabao 3-1 kabla ya kuibamiza City bao 1-0 katika mechi ya pili.
Mashujaa ambao mara kadhaa wamekuwa wakisikika kwenye mechi za mtoano za Kombe la Azam (ASFC) sasa ni zamu yao kuonesha umwamba wao kwenye ‘marathon’ ya ligi ndefu dhidi ya timu za juu kabisa Tanzania Bara.
Kuonesha wamepania kufanya jambo wameimarisha benchi lao la ufundi kwa kumnasa Kocha Mkuu, Abdallah Mohamed ‘Baresi’ aliyeinusuru Tanzania Prisons msimu uliopita isishuke daraja baada ya kunyakuliwa akitokea Mlandege ya Zanzibar aliyoipa ubingwa wa
Kombe la Mapinduzi msimu uliopita.
Katika mahojiano yake hivi karibuni, Baresi alithibitisha kuwa amekwenda Mashujaa kuimarisha ushindani wa ligi, kuonesha kitu na utofauti kutoka katika timu hiyo.
Kauli yake inashabihiana na usajili walioufanya kwa kumnasa kiungo fundi kutoka Zimamoto ya Zanzibar, Hassan Hadji ‘Cheda’, kiungo mkabaji, Said Makapu kutoka Ihefu,
beki wa pembeni kutoka KMC, Ali Ramadhani ‘Oviedo’ na wengine wenye uwezo wa mapambano ya Ligi Kuu.
Lakini pia kuonesha wako makini walienda kujichimbia Zanzibar kwa takribani wiki tatu ili kujiimarisha zaidi katika mazingira tulivu na kujipanga kwa ajili ya mikiki ya msimu ujao.
JKT Tanzania ni wazoefu, walishuka mwisho wa msimu wa 2021-22 na mwisho wa msimu wa 2022-23 wakarejea Ligi Kuu kwa ajili ya msimu ujao.
Haikuwa rahisi kwani ulikuwa ni mkakati mzito uliopangwa tangu mwanzoni mwa msimu uliopita kwa kumshusha kocha Malale Hamsini kutoka Polisi Tanzania ya Ligi Kuu.
‘Kamari’ yao ya kumleta kocha kutoka Ligi Kuu kuwanoa Championship ilifaulu vizuri baada ya Malale kufanikiwa kuirejesha kwenye ligi ya ushindani wa juu kabisa nchini. Kwa namna JKT ilivyopambana kurejea chini ya Malale ni wazi imekuja kushindana na kubaki kwa misimu mingi zaidi kwenye ligi.
Ni kama ilivyojitahidi kubaki na wachezaji wake waandamizi na wa ushindani kama Anwar Kilemile, Miraji Athumani, Richard Maranya, Hassan Kapalata kuhakikisha wanakuwa msaada mkubwa kwenye mapambano ya msimu ujao.
Pia haikushangaza kuona JKT wamepigana kikumbo na Simba na mwisho kufanikiwa kumnasa mchezaji wa zamani wa Wekundu hao, Yanga, Mtibwa Sugar na Ruvu
Shooting, Hassan Dilunga kuimarisha safu yao ya kiungo katika eneo la ubunifu.
Wameonesha wako makini mno kuelekea msimu ujao na haitakuwa rahisi kushuka mapema kama ilivyokuwa misimu iliyopita hivyo timu kongwe na zile za madaraja ya
kati zijiandae kwa upinzani mzito wa maafande hao.
Tabora United, wawakilishi pekee wa Tabora katika ligi kwa muda mrefu wamekuwa ‘wakikichafua’ kwenye Championship lakini safari hii ndio imekuwa nafasi yao kushindana Ligi Kuu msimu ujao.
Tabora kama ilivyo Mashujaa nao wameamua kumshusha Mserbia, Goran Kopunovic aliyewahi kuifundisha Simba miaka ya nyuma kuja kutetea ndoto zao msimu ujao.
Kopunovic ni mzoefu wa soka la Afrika lakini pia anafahamu ugumu wa soka la Tanzania kwa kipindi alichowahi kuhudumu Simba, hivyo kwa kifupi unaweza kusema wamelamba karata dume kuelekea msimu wao wa kwanza Ligi Kuu.
Lakini pia si umesikia waliizidi kete Simba na kumsajili kipa wa Enyimba ya Nigeria, John Noble? Sasa hii inaonesha ni kiasi gani wamepanga kuleta ushindani mkubwa kabla ya ligi kuanza kwa kugombea wachezaji wazuri dhidi ya timu kubwa na kongwe.
Ingawa yupo mkongwe Jerome Lambele lakini pia imewaongeza Mutuale Ngonyani kutoka Meniema ya Congo, beki wa kati, Kelvin Pemba (Mbabane Swallows, Eswatini), mshambuliaji Eruc Okutu (Heart of Lions, Ghana).
Wengine ni Omary Seif (Rhino Rangers), Mbombo Impire (Maniema FC, Congo), Aaron Kalambo (Polisi Tanzania), kiungo mkabaji Ingoli Gideon kutoka AC Rangers ya Congo na wengine.
Ni usajili mpana, tishio wenye hisia za kuleta mapinduzi ya kweli msimu ujao kwa timu zinazopanda kushiriki ligi.
Unaweza kusema timu zote tatu zimejipanga kila kona, kila eneo na zimefanya uchunguzi kubaini michuano ikoje na wanakwenda kupambana na wachezaji wa aina gani ndio maana sajili zao zimekuwa nzito kuanzia wachezaji mpaka wakuu wa mabenchi yao ya ufundi.
Kwa mwonekano wa awali wa uundaji na urekebishaji wa vikosi vyao, ni dhahiri wamepania kuonesha kitu na kuleta utawala wao mpya dhidi ya timu zitakazokosa uvumilivu msimu ujao kwenye mbio za mechi 30 mfululizo za ligi nzima.
Miaka ya nyuma kidogo tungeshuhudia timu kama hizi zilizopanda zingezengea wachezaji wazawa wanaoachwa kwenye timu zao za ligi ili kujaribu kuleta ushindani lakini safari hii wanapambana na vigogo na wanasajili nje ya nchi kuhakikisha hawaleti unyonge.