Masumbwi

Waamuzi wa Ngumi kupigwa msasa

DAR ES SALAAM: KAMISHENI ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kwa kushirikiana na Baraza la Ngumi Duniani (WBC) pamoja na Umoja wa Ngumi Afrika (ABU), imeandaa mafunzo maalum ya kimataifa kwa waamuzi wa ngumi wa ulingoni nchini, kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwaandaa kufikia viwango vya kimataifa.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanatarajiwa kuanza rasmi Ijumaa, Juni 13 hadi Jumapili, Juni 15 katika ukumbi wa Fit Poa Gym uliopo Msasani, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa TPBRC, Emmanuel Salehe, amesema hatua hiyo inalenga kutoa elimu ya kitaalamu kwa waamuzi hao ili kuondoa changamoto zinazojitokeza wakati wa upatikanaji wa washindi kwenye mapambano ya ngumi.

“Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa mabondia kuhusu waamuzi kutoa maamuzi yasiyo ya haki kwa kumpa ushindi mpinzani licha ya kuwa mwingine ameonyesha ubora zaidi ulingoni. Tunataka kuondoa kabisa hali hiyo kwa kutoa mafunzo haya,” amesema Salehe.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yataendeshwa kwa kutumia viwango vya kimataifa vinavyotambulika na WBC pamoja na ABU, huku washiriki wakifanyiwa tathmini ya kina ya utendaji wao kwa njia ya mitihani ya nadharia na vitendo.

Kwa mujibu wa Salehe, tatizo la waamuzi kutotoa haki si jipya, bali limekuwa likijitokeza hata katika mataifa mengine ya Afrika ambapo mara nyingi mabondia wa Tanzania wanapocheza ugenini hukumbwa na changamoto ya kupewa matokeo yasiyo ya haki.

“Tuna imani kuwa baada ya mafunzo haya, tutaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa malalamiko hayo. Washiriki watakaofaulu kwa viwango vya juu watapata vyeti vya kimataifa na pia wataingizwa kwenye orodha ya waamuzi wanaotambuliwa na ABU, WBC na vyama vingine vya kimataifa,” amesema Mwenyekiti huyo.

Mafunzo haya yanatarajiwa kuwa chachu ya maboresho ya mchezo wa ngumi nchini na barani Afrika kwa ujumla, kwa kuhakikisha haki inatendeka ulingoni na kuinua kiwango cha ushindani wa mabondia.

Related Articles

Back to top button