EPL

Van Dijk afurahishwa na hamasa ya mashabiki Anfield

ENGLAND: NAHODHA wa Liverpool, Virgil van Dijk, amesema amefurahishwa na kurejea kwa hamasa na imani ya mashabiki wa klabu hiyo katika uwanja wa Anfield, kufuatia matokeo mazuri waliyoyapata katika michezo yao ya hivi karibuni ya nyumbani.

Liverpool imepata ushindi mfululizo dhidi ya Villarreal, Brighton na Chelsea katika mashindano tofauti, hali iliyorejesha hali ya kujiamini kwa kikosi hicho baada ya msimu uliopita kushindwa kutetea taji lake la Ligi Kuu England kwa kiwango kilichotarajiwa.

Ushindi wa hivi karibuni dhidi ya Chelsea ulipatikana kupitia mikwaju ya penalti kwa mabao 6-5, baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa Kombe la Ligi England uliochezwa Jumatano.

Van Dijk, mwenye umri wa miaka 35, amesema anahisi mabadiliko makubwa katika uhusiano kati ya timu na mashabiki, akieleza kuwa matokeo mazuri yamechangia kurejesha nguvu na hamasa ya mashabiki wa Anfield.

Mabadiliko hayo yanakuja wakati Liverpool ikizidi kuzoea mfumo wa kocha mpya Andoni Iraola, aliyeteuliwa mwezi Juni kuchukua nafasi ya Arne Slot aliyefutwa kazi. Iraola, aliyewahi kuinoa Bournemouth, ameanza kujenga utambulisho mpya wa kikosi hicho.

 

Katika mchezo dhidi ya Chelsea, Iraola alifanya mabadiliko saba katika kikosi chake, akiwemo kuwatumia wachezaji wanne wenye umri chini ya miaka 22. Van Dijk alisema timu ilionyesha nguvu kubwa na kufanya kazi nzuri ya kuzuia mashambulizi ya wapinzani.

Kwa sasa, Liverpool inaelekeza nguvu zake katika mchezo mgumu dhidi ya mabingwa watetezi Arsenal utakaopigwa Jumapili Novemba 01, katika uwanja wa Anfield. Van Dijk amesema kikosi hicho kinalenga kuendeleza kiwango kizuri kwa dakika zote 90 katika kila mchezo, iwe nyumbani au ugenini.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button