UEFA yatakiwa kumwadhibu Ronaldo
NAHODHA wa Ureno Cristiano Ronaldo huenda akakabiliwa na adhabu kutoka UEFA kutokana na shutuma za ‘Kukiuka huduma za matangazo’ wakati wa mechi yao ya Euro 2024 dhidi ya Slovenia.
Ronaldo mwenye miaka 39 alionekana akiwa amevaa kifaa cha kampuni ya teknolojia ya mazoezi ya mwili inayoweza kuvaliwa, WHOOP chini ya bendeji kwenye mkono wake wa kushoto, ikirekodi mapigo ya moyo ya mchezaji huyo lakini UEFA inadai Ronaldo na WHOOP sio wafadhili rasmi wa UEFA kwenye mashindano ya Euro 2024.
Aliyekuwa mkuu wa ufadhili wa kimataifa wa Visa na Coca-Cola, Ricardo Fort, katika ukurasa wake wa Instagram ameandika akiwataka UEFA kuwatoza faini Ronaldo na kampuni hiyo kutokana na tukio hilo.
“Cristiano na WHOOP wanavizia soko la Euro 2024. Ni kinyume cha sheria, mchezaji na kampuni wanapaswa kutozwa faini,” aliandika Ricardo.