Tuchel afurahia kejeli za mashabiki

RIGA: KOCHA mkuu wa timu ya taifa ya England Thomas Tuchel alionekana mwenye furaha baada ya mashabiki kuonekana wakishangilia kwa kejeli wakati kikosi cha Mjerumani huyo kilipoichapa Latvia mabao 5-0 kwenye uwanja wa Daugavas Stadionā mjini Riga nchini Latvia jana Jumanne.
Wiki iliyopita Tuchel aliwakosoa mashabiki wa England waliojitokeza kwenye Uwanja wa Wembley, akiwashutumu kwa kutojitoa vya kutosha kwa kushangilia wakati timu hiyo ilipoibuka na ushindi wa mabao 3-0 kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Wales.
Mashabiki hao walishangilia zaidi hapo jana walipokuwa wakisherehekea timu yao kujihakikishia nafasi katika Kombe la Dunia mwaka ujao nchini Marekani, Mexico na Canada huku wakisikika wakiimba ‘ sauti ya inatosha?’ kwa meneja huyo wa zamani wa Chelsea.

“Nimepata kejeli kidogo leo katika kipindi cha kwanza, na ni sawa. Ninapokea kejeli hizo vizuri. Nimefurahi. Walikuwa na sababu leo kutokana na nilivyowasema wiki iliyopita ninapokea kwa hisia Chanya”
“Naona ni ubunifu mzuri kabisa. Ilinifanya nitabasamu na hivi ndivyo inavyopaswa kuwa. Msaada wao leo ni umetusaidia sana na tuna uhakika kwamba tutapata uungwaji mkono mkubwa wakati wa Kombe la Dunia huko Amerika.” – Tuchel amesema.




