Timu ya kriketi U19 waichapa Japan

TIMU ya Taifa ya kriketi ya vijana chini ya umri wa miaka 19 (Tanzania U19) imeshinda mchezo wa Kimataifa wa kirafiki wa maandalizi ya Kombe la Dunia dhidi ya Japan U19 kwa mikimbio 81.
Tanzania iliweka alama mapema baada ya kukusanya mikimbio 204 kwa kupoteza wiketi tisa katika overs 50, ikionesha ubora wa kupiga mpira kwa kujiamini na nidhamu ya hali ya juu.
Katika kujibu, Japan U19 ilijikuta ikizama mbele ya mashambulizi makali ya watupaji wa Tanzania, waliojipanga vyema na kutumia kila nafasi kuangusha wiketi, hali iliyoihakikishia Tanzania ushindi wa kishindo na kuongeza morali kwa kikosi hicho.
Ushindi huo ni ishara tosha ya mwanzo mzuri na kasi chanya kwa vijana wa Tanzania, huku safari ya kuianza Kombe la Dunia ikiendelea kwa matumaini makubwa. Itacheza mchezo mwingine dhidi ya Ireland kesho.
Michuano hiyo ya Dunia imeandaliwa na nchi za Zimbabwe na Namibia na tayari Tanzania wako Namibia. Wakihitimisha michezo hiyo ya kirafiki wataanza michezo ya hatua ya makundi Januari 15 dhidi ya West Indies, baadaye Afrika Kusini na kuhitimisha kwa Afghanistan.




