BurudaniFilamu

The Body (El Cuerpo)

POLISI nchini Hispania, wakiongozwa na Inspekta Jaime Pena, wanapokea taarifa kutoka
katika hospitali moja, upande wa chumba cha kuhifadhia maiti, kwamba kuna mwili umetoweka kutoka ulipokuwa umehifadhiwa.

Ni leo tu mwili huu uliletwa hospitalini hapo, kibaya zaidi, licha ya uwepo wa kamera za ulinzi (CCTV) ndani ya chumba hicho na jengo zima lakini kamera hizo hazikurekodi
chochote zaidi ya kumwonesha mlinzi wa zamu, Angel Torres, akikimbia ovyo kutoka kwenye eneo lake la kazi, kabla hajagongwa na gari.

Alichokiona mlinzi huyo hakijulikani wala hakionekani! Hiki sasa ni kizungumkuti!
Marehemu ambaye mwili wake umepotea toka chumba cha kuhifadhia maiti anaitwa Mayka
Villaverde, mwanamama mfanyabiashara tajiri, ambaye ameolewa na kijana aitwaye Alex Ulloa.

Wawili hawa wamepishana sana kiumri, Mayka akiwa katika umri ambao unaanza kukimbia marathoni, Alex bado ni kijana mdogo.Ndiyo hivyo tena!

Kwa kuwa mwanamama huyu yupo vizuri sana kifedha, Alex ikambidi aifunge roho yake na kujivinjari na mwanamama huyu, wenyewe wanawaita vijana wa aina hii ‘ving’asti’ au ‘marioo’.

Katika uhusiano wao wa ndoa, mambo yanakwenda vizuri hadi siku moja ambayo macho ya Alex yanamwona msichana mrembo, Carla Miller.

Binti huyu ni mwanafunzi wa chuo kimoja ambacho Alex alialikwa, na tangu siku hiyo, wawili hao wanaendelea kuonana na kuonana hadi pale ambapo wanaonana zaidi kiasi cha
mioyo, nafsi, miili na akili zao kuunganika na kisha kuzama mapenzini moja kwa moja.

Kumbuka kwamba Alex ana mke nyumbani lakini taratibu moyo wake unahama toka kwa mwanamama huyo hadi kwa mchepuko wake Carla Miller. Siku hadi siku Alex anaanza kupoteza upendo kwa mkewe wa ndoa, na mke anahisi kabisa kuwa anaibiwa.

Lakini ndiyo hivyo tena, Alex hakumpenda Mayka ila fedha ndizo zimewaunganisha. Sasa changamoto inajitokeza, mchepuko unamtaka Alex achague moja, yeye au mkewe. Na kama atamchagua yeye basi ampe talaka mkewe ili wayafurahie vizuri mapenzi yao bila
bughudha za mwanamke mwingine.

Dah! Huu sasa ni mtihani mzito! Alex hawezi kumpa talaka mkewe wakati ndiye anayemtegemea kifedha, maana yeye hali yake ni pangu pakavu tia mchuzi.

Lakini ukweli bado unasimama pale pale, kihisia Alex amezama kwenye penzi la mchepuko lakini bado anazihitaji fedha za mkewe wa ndoa, jambo linalomvuruga mno.

Je, asimame na penzi la mchepuko huku akizikosa fedha au asimame na mkewe ili aendelee kutumbua maisha? Hivi amwache nani kati ya hawa wawili?

Kwani penzi la mchepuko analihitaji sana na fedha za mkewe anazihitaji pia! Ukisikia karamu mbili zilimshinda fisi ndiyo kama hivi!. Baada ya kutafakari kwa kina sasa Alex
anaamua kumtilia sumu mkewe kwenye mvinyo maana hana njia nyingine ya kujinasua toka kwenye mtihani huu mgumu.

Anahitaji kubaki na vyote, mchepuko na utajiri. Anaamini akishamuua mwanamama Mayka
atarithi mali zake ambazo atazitumbua akiwa na mchepuko wake.

Dah… Mke anaipokea bilauri ya mvinyo wenye tone la sumu ndani yake, mvinyo utakaompa malalo ya milele huku akisindikizwa na mapambio ya nyimbo za huzuni, na anaunywa mvinyo wote.

Ooh… sasa inabaki historia kuwa aliwahi kuwepo mwanamama tajiri Mayka Villaverde. Baada ya polisi kuuchukua mwili wake, ndugu tu wanabaki kumliwaza Alex ingawa yeye
anajua ni nini amekifanya kwa mkewe.

Kibaya ni kwamba, Alex hasubiri hata mkewe azikwe kwani usiku huo huo anasafiri umbali mrefu kwenda kumtembelea mchepuko wake ili apate furaha ya penzi siku ya kwanza tu ya uhuru wao baada ya mkewe kufa, maana kizuizi kikubwa kilikuwa ni mke na sasa atapata muda mwingi na mchepuko.

Haikuchukua muda simu yake inaita na anapewa taarifa kuwa mwili wa mkewe umetoweka
toka katika chumba cha kuhifadhia maiti na haujulikani ulipo.

Nani ameuchukua? Kila mtu hajui! Kwa lengo gani? Haieleweki! Hata polisi  amechanganyikiwa!

Sasa kitumbua kinaingia mchanga asubuhi ya njaa kali. Alex hana namna tena, inabidi aende hospitali kushuhudia kwa macho yake ikiwa ni kweli maneno aliyoambiwa kwenye
simu ni ya kweli au la.

Anapatwa na mshtuko anapogundua ni kweli mwili wa mkewe haupo hospitalini wakati ni yeye aliyeuleta hapo na alihakikisha kuwa mkewe kafa. Imekuwaje tena mwili wake haupo? Nani kauchukua?

Sasa Alex anaingia kwenye dimbwi la mawazo, anawaza kuwa labda pale alipompa mkewe glasi ya mvinyo wenye sumu huenda alishtuka akabadilisha glasi. Labda hakufa! Lakini haiwezekani!

Aliitumia glasi ile ile aliyompa, hata yeye alimshuhudia kwa macho yake. Au labda kuna mtu alikuja akauchukua mwili wa mkewe na kuondoka nao. Je, ni nani mtu huyo?Haiwezekani pia!

Au labda kumbukumbu zake zimepotea, huenda ni yeye mwenyewe ambaye alikuja akauchukua mwili huo na kuondoka nao! Lakini hata hilo pia haliwezekani! Hawezi kufanya
hivyo. Kwa nini auchukue?

Aupeleke wapi wakati alihitaji kufurahia penzi lake na mchepuko wake! Lakini… hebu ngoja
kwanza… au labda mkewe hakuwa amekufa ila aliigiza kwa kuwa alijua mumewe anamsaliti na hivyo akatafuta namna ya kulipa kisasi?… Hii ni sinema yenye taharuki ya dakika 107 iliyotoka mwaka 2012 nchini Hispania ikiongozwa na Oriol Paulo.

Sinema hii iliwavutia watayarishaji wa sinema kutengeneza sinema nyingine kwa kutumia
kisa cha sinema hii. Huko Tamil- Kannada kulitengenezwa sinema ya ‘Game’ iliyotoka mwaka 2016.

Wakorea nao wakatengeneza sinema ya ‘The Vanished’ iliyotoka mwaka 2018, na mwaka 2019 ilitengenezwa sinema huko India na Jeethu Joseph inayoitwa ‘The Body’ iliyowashirikisha mastaa..

Related Articles

Back to top button